Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamisi Kigwangalla akizungumza na Balozi wa China nchini Tanzania, Ms.Wng Ke, kuelezea utayari wa Tanzania kupokea Watalii kutoka nchini china wakati huu wa janga la Corona. Dkt. Kigwangalla amekua akifanya mikutano na mabalozi wa nchi mbalimbali ambazo ni masoko makuu ya utalii nchini Tanzania.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamisi Kigwangalla akizungumza na Balozi wa India nchini Tanzania, Sanjiv Kohli kuelezea utayari wa Tanzania kupokea Watalii kutoka nchini India wakati huu wa janga la Corona.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamisi Kigwangalla akizungumza Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Manfredo Fanti kuelezea utayari wa Tanzania kupokea Watalii kutoka nchi za Umoja wa Ulaya wakati huu wa janga la Corona.
Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Manfredo Fanti kuelezea akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla mara baada ya mazungumzo kuhusu utayari wa Tanzania kupokea Watalii kutoka nchi za Umoja wa Ulaya wakati huu wa janga la Corona. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Maliasili wa Ubalozi huo Bi. Correia Nunes.
Picha/ Aron Msigwa – WMU.
***************************
Na. Aron Msigwa – WMU.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa Tanzania iko tayari kupokea watalii kutoka China, India na mataifa mengine ambayo yameruhusu raia wake kusafiri nje ya nchi zao.
Dkt. Kigwangalla ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na Balozi wa China nchini Tanzania, Ms.Wng Ke, Balozi wa India nchini Tanzania, Sanjiv Kohli na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Manfredo Fanti.
Akizungumza na mabalozi hao amesema Tanzania imekwisha fungua anga na kuruhusu ndege za abiria za kimataifa kutua hali iliyochangia kufunguka kwa Sekta ya Utalii kutokana na kuwepo kwa utayari, mazingira salama na maandalizi mazuri ya kupokea na kuhudumia watalii watakaowasili nchini wakati huu wa janga la Corona.
Dkt. Kigwangalla amesema ameamua kukutana na kuzungumza na mabalozi hao kuwaelezea utayari wa Tanzania kupokea watalii na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania kufungua Sekta ya Utalii wakati huu wa janga la Corona.
Aidha, amesema ameamua kukutana na mabalozi hao kwa kuwa nchi zao zinaleta watalii wengi Tanzania pia mabalozi hao nafasi kubwa ya ushawishi na uwezo wa kuwahamasisha mawakala wa Utalii, makampuni ya huduma za utalii na raia wa nchi zao kufanya safari za kitalii nchini Tanzania.
Amewaeleza mabalozi hao kuwa Tanzania ilichukua hatua mbalimbali kukabiliana na janga la Corona ikiwemo uzingatiaji wa masharti na matakwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Mamlaka za Afya nchini kuwaelimisha wananchi na kuwasisitiza kuzingatia kanuni za afya zikiwemo za uvaaji wa barakoa, matumizi ya vitakasa mikono, unawaji wa mikono mara kwa mara na kuepuka misongamano hatarishi hali iliyochangia kuwepo kwa maambukizi madogo ya ugonjwa wa Corona.
Dkt. Kigwangalla amebainisha kuwa Tanzania haikuchukua hatua kali za kuwafungia watu majumbani (Lockdown) kama yalivyofanya mataifa mengine kutokana na uchumi na shughuli za wananchi wengi kutegemea kipato cha siku kujikimu kimaisha.
Amewaeleza mabalozi hao kuwa tayari Tanzania imezindundua mwongozo wa Taifa wa uendeshaji wa Huduma na Biashara ya Utalii ambao kulinda afya na usalama wa wadau wote wanaojihusisha na biashara ya utalii katika kipindi hiki cha janga la Corona.
Dkt. Kigwangalla amewaeleza mabalozi hao kuwa watalii wote wanaowasili Tanzania katika kipindi hiki cha janga la Corona watakuwa salama kutokana na uwepo wa mwongozo kwa kuwa huo kwa kuwa unatoa usimamizi kwenye viwanja vya ndege, hoteli za kitalii, watoa huduma za utalii, upimaji wa afya za wahudumu na wageni wote wanaoingia nchini pamoja kukusanya taarifa za wasafiri wote wanaoingia nchini Tanzania.
Dkt. Kigwangalla amewahakikishia mabalozi hao kuwa mifumo ya huduma za afya na dharula nchini Tanzania iko tayari kuhudumia watalii watakaokuwa wakiwasili kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii akibainisha kuwa Tanzania ina hospitali za kisasa, maabara za upimaji zenye vifaa vyote vya huduma za dharula katika maeneo tofauti tayari kuhudumia watalii na wageni watakaoonesha dalili za kuwa na ugonjwa wa Corona.
Pia, amewaomba mabalozi hao wapange muda wa kutembelea maeneo mbalimbali yanayotumika kupokelea watalii yakiwemo ya viwanja vya ndege, hoteli za kitalii na hifadhi mbalimbali ili kujionea utayari wa Tanzania katika kuwahudumia watalii.
Kwa upande wao mabalozi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti wamemshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa juhudi anazozifanya kuhamasisha na kutangaza utalii na kuelezea hatua zilizochukuliwa na Tanzania kuonesha utayari wake wa kupokea watalii.
Wameipongeza Serikali kwa kwa juhudi kubwa za kulinda uhifadhi na kuahidi kutoa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za uhifadhi.
Mabalozi hao wamefurahishwa na uwepo wa Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji wa shughuli za Utalii Tanzania pamoja na kuridhishwa na hali ya utulivu iliyopo inayowafanya wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku.
Aidha, wameridhishwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na Tanzania kufungua anga jambo lililowezesha mashirika makubwa ya ndege ya kimataifa kuanza kurejesha safari za anga nchini Tanzania.