Waziri wa Nishati,Dkt Medard Kalemani(mwenye miwani) akiwasili kwenye kijiji cha Usagara,Wilaya ya Misungwi,Mkoa wa Mwanza,kwenye ziara ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme vijijini.
Waziri wa Nishati,Dkt Medard Kalemani(wa kwanza) akizungumza na Bi Restuta Willbad wakati alipokwenda kukagua nyumba ya mwanakijiji huyo wa kijiji cha Isamilo, Wilaya ya Misungwi,Mkoani Mwanza,
Moja ya Nyumba ambayo Waziri wa Nishati,Dkt Medard Kalemani ameikagua ambayo ipo katika kijiji cha Usagara Wilaya ya Misungwi,Mkoani Mwanza
Waziri wa Nishati,Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa kijiji cha Isamilo, Wilaya ya Misungwi,Mkoani Mwanza wakati kwenye ziara ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme vijijini
Wananchi wa kijiji cha Isamilo, Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza wakimsikiliza Waziri wa Nishati,Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati wa ziara ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme vijijini
………………………………………………………………………………………….
Hafsa Omar-Mwanza
Waziri wa Nishati,Dkt Medard Kalemani, tarehe 26 Juni mwaka huu, amefanya ziara ya nyumba kwa nyumba ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme vijijini katika Kijiji cha Usagara na Isamilo wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Katika ziara hiyo, iliyoanzia kwenye kijiji cha Usagara na kumalizia ukaguzi huo katika kijiji cha Isamilo Dkt Kalemani aliweza kukagua zaidi ya nyumba 20 kwenye vijiji hivyo.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Isamilo, alisema kuwa lengo la ziara yake ni kukagua nyumba ambazo hazijaunganishwa na umeme katika kijiji hicho na kujua sababu zilizofanya hadi sasa hazina umeme, nyumba hizo ambazo zipo pembezoni mwa barabara.
“Sasa ndugu zangu wananchi nimekuja kwa kazi moja nimekuwa nikipita kwenye barabara hii mara kwa mara lakini kila nikitupa jicho mkono wa kushoto naona nyumba zenu zote hazina umeme jambo ambalo hatuwezi kulikubali” Alisema Dkt Kalema.
Alisema, mwanzoni mwa mwaka huu alitoa agizo nyumba hizo zianze kupelekewa umeme lakini mpaka sasa bado nyumba hizo hazina umeme.
Aidha, amelitaka Shirika la Umeme Tanzanai( TANESCO) ndani ya siku saba wawe tayari wamenza kuwapelekea umeme wananchi wa vijiji hivyo.
Pia, Dkt Kalemani ametoa agizo kwa Maafisa Uhusiano wa TANESCO nchni, kuwahamasisha wananchi kuweka umeme kwenye nyumba zao na kuwaeleza taaratibu za kuingiza kwenye nyumba zao, kuwambia wananchi majukumu yao na gharama za umeme.
Vile vile, amawataka wananchi wa vijiji hivyo, kuanza mara moja kutafuta wataalamu wa kuwafanyia wiring kwenye nyumba zao ili wapelekewe umeme kwa haraka.
Aidha, amewataka wakandarasi nchini kufanya kazi kwa weledi na wasipofanya hivyo atawasimisha kazi mara moja na kuwapa kazi wakandarasi wenye uwezo.
“Mkoa wa Mwanza tulikuwa na mkandarasi tumefuta kazi na tumemuweka mkandarasi mwengine kwahiyo mkandarasi yoyote anaye legalega tutamfuta kazi na tumewapa mpaka mwisho wa mwezi huu wawe wamemaliza kazi” Alisema.
Nae, Bi Restuta Willbad ambae ni mkazi wa kijiji cha Isamilo amesema kuwa,amefurahishwa na kitendo hicho cha Waziri cha kukagua nyumba zao na imewapa hamasa ya kwenda kulipia huduma ya umeme na wapo tayari kupokea huduma hiyo ambayo amesema itabadilisha Maisha yao kwa kuweza kujiajiri.