Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) Bw. Ochola Wayoga akisisitiza jambo katika mkutano na wanahabri (hawapo pichani). |
Na Mwandishi Wetu
MTANDAO wa Elimu Tanzania (TenMet) umeipongeza Serikali kwa hatua madhubuti iliyoichukua kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona nchini Tanzania, hadi sasa ambayo shule zote zinatarajiwa kufunguliwa na wanafunzi kuendelea na masomo yao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Da es Salaam, Mratibu wa TenMet Taifa, Bw. Ochola Wayoga amesema hata hivyo wakati shule zinatarajiwa kuendelea (Juni 29, 2020) wadau wote na Serikali pamoja na wazazi hawana budi kuendelea kuchukuwa tahadhari hadi hapo itakapotangazwa ugonjwa huo umetoweka kabisa nchini.
Akifafanua zaidi, Mratibu huyo wa TenMet taifa ameiomba Serikali na wadau wengine kuendelea kutakasa mazingira ya shule mara kwa mara ili kudhibiti kabisa maambukizi ya virusi vya corona na magonjwa mengine kwa ujumla.
Ameiomba Serikali kupitia sekta husika kuendelea kutoa huduma za mwongozo na ushauri mashuleni ili kuhakikisha wanafunzi na walimu wanaendelea kuwa salama na taarifa sahihi namna ya kudhibiti maambukizi.
Aidha ameipongeza Serikali kupitia sekta ya elimu ilivyojitahidi kuendelea kuwafundisha wanafunzi kwa kutumia TEHAMA kipindi chote cha likizo ya corona, na hivyo kushauri ipo haja ya serikali kuendelea kukuza na kuboresha mfumo wa TEHAMA katika kufundishia na kujifunzia.
“…Kutokana na ongezeko la uhitaji wa wanafunzi kupata elimu kupitia njia hizi (TEHAMA) ipo haja ya kuendelea kuboresha vituo vya elimu ya njia mbadala (alternative education pathways), mfano hata vyuo kama VETA hutumia mfumo huo…,” alisisitiza Bw. Wayoga.
Hata hivyo ameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu endelevu kwa jamii kuhusiana na ulinzi wa mtoto dhidi ya maambukizi ya corona na hata magonjwa mengine na pia kutoa rai kwa jamii yote kwa ujumla kuwajibika kwa kuungana na Serikali kuwalinda watoto wote.