……………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Babati
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) Mkoani Manyara inamshikilia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Maisaka kati Bakari Khatibu na katibu wa Tawi hilo Juma Swalehe wote wakazi wa wilaya ya Babati kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya sh. 200,000 kutoka kwa Mwinjilist wa kanisa la kinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) mtaa wa Komoto.
Mkuu wa Takukuru Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu aliyasema hayo mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Makungu alisema viongozi hao waliomba rushwa ya sh. 200,000 kinyume na kifungu 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Alisema wawili hao waliomba na kupokea fedha hizo kutoka kwa Mwinjilist wa kanisa la KKKT Komoto kwa maelelezo kuwa baada ya kupokea fedha hizo wangemwachia kiwanja walichokuwa wakidai kuwa ni mali ya CCM.
Alisema kuwa uchunguzi zaidi kuhusiana na uhalali wa CCM kumiliki kiwanja hicho na Mamlaka ya viongozi hao kuhusiana na mali za chama unaendelea na mara utakapokamilika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Rai yetu kwa viongozi wachache ndani ya chama tawala hasa wa ngazi za chini wenye utajiri wa fikra haba wanaopitapita wakiwaaminisha wananchi kuwa hawawezi kuguswa na Takukuru kwa kua chama kilichowaajiri ndicho kinaongoza serikali,” alisema Makungu.
Aliwakumbusha viongozi wa aina hiyo ibara ya 13(1) (5) ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na kunuu” Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria bila kuzingatia utaifa wao, kabila, pahala walipotokea, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini, jinsia au hali ya maisha,”Alisisitiza
Alisema kwa msingi huo katiba uwe wa chama tawala au vyama vingine vya upinzani, sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 inakuhusu ili mradi nafasi yako iwe ni kutelekeza majukumu yanayohusiana na umma wa watanzania hivyo watendaji ndani ya chama tawala ni vyema pia wakafahamu kuwa hawako juu ya sheria na anayekiuka hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yake kama ilivyo kwa watu wengine.