…………………………………………………………………………………
NA MWANDISHI WETU-MOROGORO
Daktari Mshauri Mwandamizi wa Magonjwa ya Ndani na Moyo, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ambaye pia ni Mhadhiri wa vyuo vikuu mbali mbali vya tiba, Profesa Harun Nyagori, ameshauri taasisi za vyuo vikuu vya Afya nchini Tanzania, pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), kumpatia tuzo maalumu ya heshima, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa ajili ya kutambua mchango wake katika kupambana na janga la Corona.
Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Morogoro jana, Profesa Nyagori ambaye amewahi kutunukiwa tuzo mbali mbali za kimataifa zilizotambua mchango wake katika tafiti za maradhi ya moyo barani afrika, alisema kuwa kuna haja ya kutambua mchango mkubwa uliotukuka alioutoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, kwa mbinu za kipekee alizozitumia kupambana na janga la mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na Virus vya Corona.
“ Nikiwa kama mtaalamu niliyebobea katika masuala ya tiba ya maradhi ya binadamu, ninampongeza sana Rais Dkt John Magufuli, kwa namna alivyoweza kutoa mchango wake mkubwa kwa Watanzania na Ulimwengu kwa ujumla katika kupambana na janga la mlipuko wa ugonjwa wa Corona na ninatoa wito kwa taasisi za vyuo vikuu vya Afya hapa nchini na Shirika la Afya la Duniani (WHO) kumpatia tuzo maalumu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli kwa kutambua mchango wake.”
Profesa Nyagori aliongeza kusema kuwa ugonjwa wa Corona ulipoingia kwa mara ya kwanza hapa nchini, wananchi wengi walijawa na hofu kubwa juu ya athari za ugonjwa huo na hivyo walihitaji sana kumpata mtu wa kuwatoa hofu hiyo.
“ Msongo wa mawazo (stress) unasababisha uwezo wa kinga mwilini kushindwa kupigana na maradhi na hivyo kinga za mwili kupungua ambapo kichocheo cha corticosteroid kinachozalishwa kwenye mwili kinaweza kuwa kisababishi kikubwa cha kupunguza kinga za mwili. Hofu huchukua nafasi kubwa sana katika kumfanya mtu kupata athari kubwa za ugonjwa fulani. Kisayansi hofu husababisha kinga za mwili wa biniadamu kushuka na hivyo kumfanya kuwa rahisi kuambukizwa na kushambuliwa na maradhi sambamba na kupata athari kubwa zaidi. Rais Dkt John Magufuli amefanya kazi kubwa kuwajengea ujasiri Watanzania kutokuwa na hofu kubwa juu ya ugonjwa huu wa Corona, huku wakichukua taadhari za kiafya ambazo wataalam wa Afya wanazitoa. Hatua hii imeepusha kwa kiwango kikubwa, athari ambazo zingetokana na ugonjwa huu.” Alisema Profesa Nyagori.
Profesa Nyagori aliongeza kusema kuwa majirani zetu na nchi nyingine nyingi ulimwenguni zimejikuta katika sintofahamu kubwa kutokana na janga la Corona kwa sababu hazikuwa na viongozi mathubuti, wenye msimamo, mbinu na ubunifu wa namna sahihi ya kupambana na janga hili kwa njia ya kisaikolojia kama ambavyo Rais Magufuli amekuwa nao.
KUHUSU KARANTINI
Akizungumzia kuhusu mbinu ya kujifungia ndani (karantini) kama njia ya kuepuka na kuepusha kusambaa kwa maambuki ya virusi vya Covid-19, Profesa Nyagoli alisema kuwa mbinu hiyo endapo kama ingetumika, ingelikuwa na madhara makubwa kuliko faida.
“ Hatua ya Rais Magufuli kutokubaliana na mbinu ya kujifungia ndani (Lockdown), imesaidia sana katika kuwafanya watanzania kuendelea kutafuta fedha ambazo zimewawesha kumudu kupata milo yenye lishe ambayo kimsingi imeimarisha kinga zao na kufanya isiwe rahisi kushambuliwa na maradhi Corona.
“Kujifungia ndani licha ya kisaikolojia kuongeza wasiwasi, lakini pia humfanya mtu kutopata fursa ya kutafuta pesa na hivyo kutomudu kupata mahitaji muhimu ikiwemo vyakula mchanganyiko ambavyo ni muhimu kwa lishe inayoimarisha kinga mfano vitamin na madini mbalimbali.” Alisema Profesa Harun Nyagoli. MWISHO.