Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe, Bw. Pius Kazeze, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa, wakati Naibu Waziri huyo alipokuwa akikagua hatua za uboreshaji wa kiwanja hicho, mkoani Mbeya
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoka kukagua eneo linalongezwa kwa ajili ya usalama wa ndege zinazoruka na kutua katika Kiwanja cha Ndege cha Songwe, mkoani Mbeya
Muonekano wa jengo la abiria la sasa linalotumika, jengo jipya la abiria linalojengwa ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria laki tano kwa mwaka na barabara ya zege ya kutua na kuruka ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Songwe, mkoani Mbeya. Uboreshaji wa kiwanja hicho unagharimu bilioni 14.7
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akikagua uimara wa barabara ya zege iliyopo katika maegesho ya ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Songwe, mkoani Mbeya.
Kazi za uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe zikiendelea, mkoani Mbeya.
*****************************************
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amemtaka mkandarasi China – Geo Engineering Corporation kuzingatia viwango vya ubora wa kimataifa katika uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe.
Aidha, amemuagiza kuongeza vifaa muhimu vyote katika eneo la kazi na wataalamu wa kutosha ili waweze kufanikisha utendaji kazi usiku na mchana kwa muda waliopangiwa wa miezi nane.
Kwandikwa alisema hayo akiwa mkoani Mbeya, alipofanya ziara ya kukagua hatua iliyofikiwa ya mradi huo utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 14.7 ambapo fedha hizo zinatolewa na Serikali kwa asilimia 100.
“Nimekuja kuona maendeleo ya uwanja huu na ninafahamu kuwa hapa kumekuwa na changamoto ya mvua na kusababisha maeneo mengi ya mradi kukwama sasa mvua imepungua, naagiza kazi iendelee kwa kasi zaidi”, amesema Naibu Waziri huyo.
Alifafanua kuwa lengo la Serikali ni kuufanya uwanja huo kuwa ni wa kimataifa na wenye sifa zote za kuruhusu ndege kubwa kuruka na kutua na kutumika usiku na mchana.
“Huu uwanja tunahitaji utumike kimataifa kama viwanja vingine na ndio maana maboresho tunayofanya yanahusisha na utoaji wa barabara ya zamani ya kuruka na kutua ndege yote iliyokuwepo uwanjani hapo na kuweka tabaka jipya la lami ya zege imara ili ndege kubwa zitue bila tatizo lolote, taa za usiku na uzio”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Kwandikwa alisema Serikali inategemea kuibua shughuli nyingi za kimaendeleo katika Mkoa wa Mbeya kupitia kiwanja hicho kwa kuwa mkoa unavutia kuwa na vitu vingi vya kufanya hususani biashara.
Awali akitoa taarifa ya mradi Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Mbeya, Mhandisi Eliazary Rweikiza, alisema kuwa kazi ya usimamizi wa uboreshaji wa kiwanja hicho unasimamiwa na TECU na kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa tabaka jipya la lami, uzio, uwekaji taa za kuongezea ndege na ujenzi wa eneo la usalama mwisho na mwanzo wa uwanja.
Uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe ni moja ya mkakati wa Serikali wa ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege 11 nchini vikiwemo Viwanja vya Songea, Shinyanga, Mtwara, Kigoma, Sumbawanga, Tabora, Iringa na Musoma ambavyo vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.