Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu akikagua ufuta kwenye ghala la Huru Amcos lililopo Kijiji cha Shangani kata ya Michenjele ambapo amewaasa Wakulima wa Ufuta kuzingatia ubora na kuuza ufuta wao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
…………………………………………………………………………………………..
~ Kuhakikisha wanauza Ufuta ghalani
~ Kuzingatia ubora
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Wakulima wa zao la Ufuta wameaswa kuuza Ufuta wao kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuzingatia ubora na si vinginevyo.
Hayo yamejiri kwenye ziara aliyoifanya Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu ya kukagua upokeaji Ufuta alipotembelea Maghala ya vyama vya msingi vya Huru na Ruvuma.
“Nimefanya ziara kukagua zoezi zima la upokeaji wa Ufuta kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo nawasihi Wakulima wa Ufuta Tarafa ya Mihambwe Kuhakikisha hawauzi Ufuta wao nje ya mfumo wa stakabadhi ghalani ili wanufaike na jasho la kazi yao na wapeleke Ufuta Safi ghalani kivutio kwa wanunuzi wa bei kubwa.” alisisitiza Gavana Shilatu.
Nae Mkulima wa Ufuta Adamu Abdallah Mwema alimshukuru Rais Magufuli kwa kuboresha zao la ufuta kulifanya lenye tija na kuwasihi Wakulima kuongeza bidii ya uzalishaji.
“Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kutuboreshea ufuta, kazi kwetu Wakulima kujibidiisha zaidi kujiletea maendeleo.” Alisema Mkulima Mwema mkazi Kijiji cha Michenjele kilichopo kata ya Michenjele.
Kwa msimu wa mwaka huu 2020/2021 Tarafa ya Mihambwe inatarajia kuuza Ufuta wa kiasi kisichopungua tani 150 zaidi ya tani 70 zilizopatikana msimu wa mwaka Jana 2019/2021.