Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizungumza na viongozi wa Wizara mbalimbali na wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakati wa Uzinduzi wa Muongozo wa Uratibu wa Masirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara leo (17/06/2020) Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara wa Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akitoa maelezo kuhusu Muongozo wa Uratibu wa Mashrika Yasiyo ya Kiserikali wakati wa Uzinduzi wa Muongozo huo leo (17/06/2020)Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt. Richard Sambaiga akieleza jambo kuhusu utaribu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika uzinduzi wa Muongozo wa Uratibu wa Masirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara leo (17/06/2020)Jijini Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wa pili kulia, Katibu Mkuu Wizara wa Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya kserikali Dkt. Richard Sambaiga (wa pili kushoto) na Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao wakionesha nakala ya Muongozo wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara mara baada ya kuzinduliwa leo (17/06/2020) Jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa hafla ya Uzinduzi Muongozo wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu leo (17/06/2020) jijini Dodoma.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
………………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuzingatia Uwazi katika matumizi ya fedha za wafadhili ili kufanikisha malengo ya fedha hizo ambayo ni kuleta maendeleo kwa Wananchi.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo (17/06/2020) jijini Doddoma wakati akizindua Muongozo wa uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara ambapo amesema fedha nyingi zinaingia nchini kwa ajili ya kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo lakini baadhi ya mashirika hayaweki wazi takwimu za mapato na matumizi fedha hizo.
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema lengo la mwongozo sio kuyabana Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini bali ni kuhakikisha Wananchi wananufaika na fedha zilizoombwa na Mashirika hayo kwa ajaili maendeleo ya wananchi husika.
Akitoa Mfano, amesema katika Kipindi cha Mwezi Desemba, 2018 hadi Mei 2020 Jumla shilingi Trillioni 3.9 ziliingia nchini kupitia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya mbalimbali ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
“Lazima tujue Mashirika yanaingiza kiasi gani cha fedha na zinatumikaje katika kuleta maendeleo kama ilivyokusudiwa katika maombi ya fedha hizo” alisisitiza Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy ameyaelekeza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuzingatia maelekezo ya muongozo huo, kwa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia utaalamu wa Kisekta kwa kila afua itakayokuwa inatekelezwa na mashirika hayo, ikiwa ni pamoja na kuomba vibali kutoka kwenye Sekta husika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara wa Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema kuwa Muongozo huo utaimarisha mazingira na jitihada za kuboresha ya ufanyaji kazi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili yaweze kutoa machango wake katka maendeleo ya taifa.
“Katika Muongozo huu umeeleza kwa kifupi Sheria, taratibu na kanuni zinazotakiwa kufuatwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuhakikisha yanatimiza wajibu wake na kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt. Richard Sambaiga amesema kuwa Muongozo huo utasaidia Uratibu mzuri kwa Mashirika hayo kutokana na ongezeko la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambalo limeongeza changamoto za kiutendaji kwa Mashirika yasiyo ya kiserikali nchini.
Amesema awali kulikuwa na changamoto ya usajili na uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutokana na kuwajibika kwa Mamlaka zaidi ya moja na hivyo kusababisha usumbufu kwa wadau.