Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wadau wote wanaotoa huduma Tembezi za Afya kuunganisha nguvu kwa pamoja ili huduma hiyo iweze kufikishwa katika Halmashauri zote Nchini.
Dkt.Gwajima ameyasema hayo wakati wa kikao cha wadau wa Afya kuwasilisha Taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi kilichofanyika katika Ukumbi wa Takwimu Jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho Dkt. Gwajima amesema huduma Tembezi za Afya ni muhimu kufikishwa katika Ngazi ya Jamii ili wananchi waweze kupata matibabu kutoka kwa madaktari bingwa tena kwa gharama nafuu.
“Huduma hizi zimekuwa zikitolewa na Taasisi tofauti kwa nyakati tofauti na kila Taasisi analenga eneo Fulani ambalo anachagua hivyo kuna maeneo ambayo yamekuwa yakinufaika na huduma hizi mara kwa mara lakini kuna sehemu nyingine hazifikiwi kabisa sasa ni umefika wakati wa kukaa pamoja na kuunganisha nguvu ya wadau wote pamoja na Serikali na kupelekwa huduma hii katika Halmashauri zote ili kila mwananchi mwenye uhitaji anufaike nayo”
Kupitia Kikao hiki cha leo tutaunda Kamati ya Uendeshaji ambayo itahusisha Wataalamu wa OR-TAMISEMI, Wizara ya Afya, Asassi zisizo za Kiserikali pamoja na wadau wanaotekeleza Afua za Afya ambao watakuja na hadidu za rejea zitakazotuongoza katika kutekeleza azima yetu hii kwa ufanisi aliongeza Dkt.Gwajima.
Pia Dkt. Gwajima alisema kuwa “Tunajua tuna vituo vya kutolea huduma vya lakini si wakati wote vituo hivyo vinakuwa na madaktari Bingwa na kwa mwananchi wa kawaidia kusafiri mpaka kukutana na madaktari bingwa ni gharama hivyo tukisogeza huduma hizi tutawatibu wananchi wetu hata yale magonjwa ambayo walikuwa wameyakatia tamaa”Alisema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima aliongeza kuwa Huduma hizi Tembezi zina faida zake kwanza gharama za kuwekeza katika huduma hii ni ndogo lakini inawafikia watu wengi tena kwa muda mfupi. Unafuu huu wa gharama sio kwa sisi kama watoa huduma lakini pia kwa wagonjwa ambao ndio wanufaika wa huduma hii yaani ugonjwa ambao angeweza kutumia zaidi ya shilingi milioni moja anaweza kupata huduma hiyo hiyo kupitia Kliniki Tembezi kwa elfu thelathini tu.
“Huduma tembezi ni msaada kwa wanyonge, wananchi wanaugua magonjwa makubwa ambayo hata akisafiri kumfuata Daktari Bingwa anaweza akafia njiani kabla hata hajakutana na huyo Daktari, kupitia huduma hii watakutanishwa na Madaktari bingwa kwa urahisi na nafuu zaidi na hapo tutakuwa tumegusa maisha ya watanzania na kuwaongezea siku za kuishi maana wangeweza kufa kwa kukosa huduma za Afya stahiki kwa magonjwa yanayowasumbua” Alisema Dkt. Gwajima.
Tusipowafuata na kuwatibu wananchi wataendelea kunywa miti shamba na kwenda kwa waganga na hata wakati mwingine kupoteza maisha yao kwa kukosa matibabu stahiki hebu tuwafikie wote kupitia huduma hii ya Kliniki Tembezi alimalizia Dkt. Gwajima.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainabu Chaula amesema agenda kuu katika Sekta la Afya ni Huduma ya Afya kwa Wote na hakuna mtu atakayeachwa nyuma hivyo ni lazima tuifikishe huduma hii ya Kliniki Tembezi kwa wananchi wote.
“Tunapoelekea katika Uchumi wa Kati ni wajibu wetu kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na Afya Njema ili aweze kushiriki kikamilifu katika kujitafutia kipato sasa hii kazi kwetu itakua rahisi tukiunganisha nguvu na rasilimali katika kutoa huduma hii ya Afya Tembezi tushirikiane kikamilifu kuleta tabasamu kwa watanzania” Alisema Dkt. Chaula.
Akiwasilisha Taarifa ya Huduma za Afya Tembezi Mratibu wa Huduma hiyo Dkt. Mombeki Domisian amesema tangu walipoanza kutoa huduma hii katika Mkoa wa Singida imeokoa maisha ya watanzania, imetoa elimu ya Kinga, imepeleka utaalamu na zaidi imetoa ushauri kwa wagonjwa kulingana na ugonjwa husika.