………………………………………………..
Na Masanja Mabula , Zanzibar.
ASASI za kiraia Zanzibar zimeungana kwa pamoja kuadhimisha siku ya Mtoto Afrika kwa ajili ya kujadili na kutathimini hali ya udhalilishaji wa Watoto Zanzibar.
Meneja Sera na Utetezi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA Zanzibar, bi Salma Lusangi alisema maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa watu wenye ulemavu Zanzibar (UWZ) .
Mkutano huo wa Maadhimisho uliwashirikisha maafisa kadhaa kutoka sekta binafsi na sekta za umma akiwemo afisa kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mashtaka Zanzibar (DPP), Mahakama, Wizara ya kazi, uwezeshaji, wanawake na watoto, maafisa dawati, wanaharakati wa ukatili wa kijinsia kutoka mikoa ya Zanzibar.
Alisema anaamini ushiriki wa wadau hao utaweza kuleta nguvu za pamoja katika kupambana na ukatili wa kijinsia kwa watoto Zanzibar kwani kupitia mkutano huo utatoa fursa kwa wadau kujadiliana pamoja kuhusu njia mbalil mbali zinazohusiana na haki za mtoto pamoja na kupanga mikakati ya kumlinda mtoto kuepukana na matendo maovu.
“Tunaamini ushiriki wa Asasi za kiraia utasaidia kuleta nguvu za pamoja katika kupamba na matendo ya udhalilishaji kwa watoto wetu Zanzibar,” alisema Lusangi.
Lusangi aliongeza kuwa miongoni mwa Asisi zitakazo shiriki katika mkutano huo ni pamoja na Chama cha Waandishi Wahabari Wanawake Tanzania (TAMWA),Zanzibar, Mtandao wa Kijinsia Zanzibar “ZANZIBAR GENDER COALITION” (ZGC), Chama cha wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuia ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), nk.
Aidha Lusangi alieleza kuwa kaulimbiu ya Asasi hizo za kiraia kwa mwaka huu ni “Mifumo rafiki ya upatikaji wa haki ya mtoto ni Msingi Imara wa Kulinda Haki zao”
Juni 16 kila mwaka bara la Afrika huadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika tangu kuidhinishwa kwa siku hiyo na Umoja wa Afrika mwaka 1991 kama sehemu ya kuwakumbuka na kutambua mchango wa watoto waliopoteza maisha katika mauaji yaliyotokea huko Soweto, Afrika ya Kusini wakati watoto walipoandamana kudai haki zao za msingi.
picha.
wadau wa masuala ya utetezi wa haki ya mtoto wakishiriki mkutano wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa afrika zanzibar