Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akieleza jambo, wakati wa kikao cha Kamati za Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya afua za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU.
Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii wakisikiliza taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya afua za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU kutoka kwa Waziri wa Afya.
Mkuu wa Kitengo cha Kinga Mpango wa taifa wa kudhibiti UKIMWI, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Magreth Kagashe akijibu swali lililoulizwa mjumbe wakati wa kikao cha kamati ya kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii.
Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii Mhe. Oscar Rwegasira Mukasa akisikiliza kwa makini taarifa kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya afua za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU iliyosomwa na Waziri wa Afya.
Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akifafanua jambo mbele ya wajumbe wa kamati ya Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii.
******************************
Na WAMJW-DOM.
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza makubaliano ya kitaifa na kimataifa juu ya mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini kwa kuweka mipango inayolenga kuzuia maambukizi mapya na kutoa huduma za tiba na matunzo kwa wanaoishi na VVU.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo Ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika kikao cha Kamati za Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya afua za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU, katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau tumekuwa na mwitikio wa pamoja katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini kwa kuweka Mipango ya Kitaifa ambayo imekuwa ikilenga katika kuzuia maambukizi mapya na kutoa huduma za tiba na matunzo kwa wanaoishi na VVU” alisema.
Aliweka wazi kuwa, baadhi ya malengo yaliyotolewa ni Pamoja na, kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2020 na kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030, huku akisisitiza lengo kuu ni kuhakikisha uwepo wa uwajibikaji katika utoaji wa huduma bora za kinga dhidi ya VVU.
Aliendelea kusema kuwa, makubaliano haya yalianzishwa mwaka 2017 na nchi wanachama wa umoja wa mataifa, wahisani, asasi za kiraia na wadau mbali yakihusisha nchi 25 zenye viwango vikubwa vya maambukizi ya VVU ikiwemo Tanzania.
Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa, Utekelezaji wa makubaliano haya umekuwa ukipimwa kuanzia 2018 kupitia kadi maalumu ambayo inaonyesha taarifa muhimu za mwenendo wa utekelezaji wa malengo ya kitaifa yaliyowekwa na n chi kama vile huduma jumuishi za kinga kwa vijana rikabalehe na wanawake vijana (miaka 15-24) pamoja na wenzi wao.