***************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura imeongezeka ambapo wapiga kura halali kwa mwaka huu ni 29,804,992 ikilinganishwa na wapiga kura 23,161,440 wa mwaka 2015.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Tume inaendelea na uchambuzi wa taarifa za wapiga kura waliojiandikisha na baada ya zoezi hilo kukamilika, Daftari la mwisho litakalotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 litaandaliwa na kuwekwa wazi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 15, 2020) bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge, ambapo amesema kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea vema na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Amesema takwimu za awamu ya kwanza na ya pili, zinaonesha kuwa wapiga kura wapya walioandikishwa ni 7,326,552, wapiga kura walioboresha taarifa zao ni 3,548,846 na wapiga kura 30,487 wamepoteza sifa.
Amesema zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa awamu ya kwanza lilianza rasmi Julai 18, 2019 na kukamilika Februari 23, 2020 kwa nchi nzima wakati awamu ya pili ilianza Aprili 17, 2020 na kukamilika Mei 5, 2020.
“Hivi sasa, pamoja na mambo mengine Tume imekamilisha matakwa ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya kufanya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya uchaguzi mkuu mmoja na mwingine.”
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi wazingatie Katiba, sheria, kanuni na miongozo iliyopo katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.
Vilevile, Waziri Mkuu amewasihi viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla waendelee kulinda amani na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki na wakati wa uchaguzi mkuu.