Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hati ya Shule ya Sekondri ya Wasichana ya Bunge kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai (wa pili kushoto) wakati alipoweka jiwe la msingi na kukabidhiwa shule hiyo iliyopo Kikombo Dodoma, Juni 14, 2020. Shule hiyo imejengwa na wabunge na kutolewa kwa Serikali. Wa pili kulia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga, na wa watatu kulia ni Mbunge wa Urambo na Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania , Margaret Sitta na kushoto ni Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipanda mti wakati alipoweka jiwe la msingi la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge katika eneo la Kikombo Dodoma, Juni 14, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua majengo ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Bunge iliyopo Kikombo Dodoma Juni 14, 2020. Kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai (wa tatu kulia) wakiweka jiwe la Msingi la Shule ya Sekondari ya Wachana ya Bunge iliyojengwa na wabunge na kukabidhiwa kwa Serikali Juni 14, 2020. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo na wa pili kulia ni Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson Mwansasu. Kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako na wapili kushoto ni Mbunge wa Urambo na Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake, Margaret Sitta. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Jengo la Utawala la Shule ya Sekondari ya Bunge ambayo imejengwa na Wabunge na kukabidhiwa kwa Serikali Juni 14, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiagana na Spika wa Bunge Job Ndugai (kushoto) na Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (katikati) baada ya kuweka jiwe la msingi la Shule ya Sekondari ya Wasicha ya Bunge na kukabidhiwa shule hiyo iliyojengwa na Wabunge katika eneo la Kikombo Dodoma, Juni 14, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
*********************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa watu wote watakaothibitika kufanya vitendo vya kuwakatisha watoto wa kike ndoto za masomo ikiwemo kuwafunga jela miaka 30.
Pia amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote nchini wahakikishe wanaendelea kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama hadi ngazi za kata kusimamia Sheria ya Elimu ya kuwalinda watoto wote wa kike walio chini ya umri wa miaka 18.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Juni 14, 2020) wakati alipoweka jiwe la msingi na kukabidhiwa shule ya sekondari ya wasichana ya Bunge High School iliyojengwa na wabunge katika Kata ya Kikombo jijini Dodoma kwa thamani ya zaidi ya sh. bilioni moja.
“Sekta ya elimu ni wakala wa mabadiliko katika jamii kiuchumi, kiteknolojia na kiutamaduni katika kuleta maendeleo ya nchi. Ninawapongeza sana waheshimiwa wabunge kwa kuamua kuwa sehemu ya wadau muhimu katika sekta ya elimu .”
Amesema utoaji wa elimu bora kwa Watanzania ni moja ya vipaumbele vya nchi katika kuleta maendeleo na kufikia malengo ya Milenia 2025, Elimu kwa wote (EFA) na Mkakati wa Kupambana na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA).
Waziri Mkuu amesema ili kuweza kufanikisha hayo wanahitaji sekta hiyo iwe bora, imara, inayokidhi mahitaji ya jamii kwa kuwapa vijana maarifa na ujuzi wa kukabiliana na matatizo ya kijamii, kitaifa na kimataifa.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali imepata mafanikio makubwa sana kwa upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya na maji, ambapo kwa sasa kuna shule za msingi 17,659 na shule za sekondari 4,883 nchi nzima zikiwemo shule za sekondari za Serikali za wasichana 156.
”Idadi hii ya shule imesaidia kutoa fursa kwa wanafunzi wengi kupata elimu nchini katika ngazi mbalimbali. Hivi sasa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi tunatekeleza mpango wa elimu bila ada kwa kutoa shilingi bilioni 22.8 kila mwezi kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapata fursa bila vikwazo.”
Amesema Serikali, itaendelea kusimamia utekelezaji wa sera ya Elimumsingi Bila Ada kwa lengo la kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu ya sekondari na stadi za kazi, kuondoa vikwazo kwa watoto wa kike kupata elimu ya sekondari, kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji pamoja na uratibu, usimamizi na tathmini ya ubora wa elimu ya sekondari.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mikakati maalum ya kuwasaidia watoto wa kwa kuhakikisha wanapata elimu bora na kutokana na mikakati hiyo idadi ya wanafunzi wa kike wanaosoma Elimu ya Juu imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka katika ngazi mbalimbali.
Mfano idadi ya wanafunzi wa kike katika Elimu ya Juu wameongezeka kutoka wanafunzi 49,959 kati ya wanafunzi 139,638 waliodahiliwa mwaka 2010/2011 hadi kufikia wanafunzi 90,159 kati ya wanafunzi 230,339 waliodahiliwa mwaka 2017/2018. “Niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwa elimu ya mtoto wa kike.”
Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu isimamie kufungua madawati ya malalamiko katika vyuo vikuu kuhusu unyanyasaji wa kijinsia. “Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wahadhiri watakaobanika kujihusisha na unyanyasaji wa kijinsia katika vyuo chini ya sheria ya Mahusiano ya kulazimisha.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) watumie shule hiyo kuwatambua wasichana wenye vipaji hususan kwa tahasusi za sayansi na kuwasaidia kuvikuza na kuviendeleza.
Amesema kwa kufanya hivyo, watakuwa wakitoa motisha kwa wanafunzi hasa wa kike na kuwatia moyo ili wayapende masomo ya sayansi na teknolojia na hatimaye kuongeza idadi ya wataalamu wa kike. Shule hiyo ni ya mchepuo wa sayansi.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge Job Ndugai amesema ujenzi wa shule hiyo ni alama kubwa iliyowekwa na wabunge wa bunge la 11 kwani wamefanya jitihada kubwa katika kujitolea kuchangia fedha zilizowezesha ujenzi wa shule hiyo.
“…Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha wabunge wa bunge la 11 kuweza kufanikisha ujenzi wa shule ya Wasichana ya Bunge ambayo itakuwa ya kidato cha tano na sita kwa mchepuo wa sayansi.”
Awali, Mwenyekiti wa Umoja wa Wapunge Wanawake Tanzania (TWPG), Margaret Sitta alitumia fursa hiyo kumshukuru Spika Ndugai kwa kuunga mkono juhudi za wabunge wanawake na hatimaye kufanikisha ujenzi wa shule hiyo.
Pia, alimshukuru na kumpongeza Spika Ndugai kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia unaendelea kuwepo bungeni. Hata hivyo ameiomba Serikali iangalie namna ya kuwawezesha wanawake wengi kuingia bungeni kwa kupitia majimbo kwani waliopo ni asilimia tisa tu ya wabunge wote wa majimbo.