Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma mapema leo.
Picha mbalimbali zikionesha Waziri Ummy Mwalimu akiwajulia hali wananchi waliojitokeza kutoa damu katika Kituo cha Damu Salama kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Meneja wa Mpango wa Damu Salama nchini Dkt. Magdalena Lyimo akifafanua jambo kwa Waziri Ummy Mwalimu wakati alipotembelea kituo cha damu salama kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
*******************************
NA WAJMW-DODOMA
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameziagiza Hospitali zote nchini za Serikali na binafsi, Zahanati na Vituo vya Afya kuacha kuwadai damu wagonjwa kabla ya kuwapa huduma.
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya wachangia damu duniani yenye kauli mbiu “Damu Salama inaokoa maisha” ambayo kitaifa yamefanyika katika kituo cha kidogo cha damu salama kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.
“Nazitaka Hospitali zote za Serikali na binafsi kuacha tabia ya kuwadai damu wagonjwa na ndugu kabla ya kumpatia mgonjwa huduma, mnatakiwa kutoa huduma kwanza na masuala ya wanandugu kuambiwa walete watu wa kuchangia damu kabla ya huduma ni kinyume na taratibu na kanuni za utoaji wa huduma za afya”. Amesisitiza Waziri Ummy.
Waziri Ummy amezitaka Hospitali zote za Serikali na binafsi na vituo vya Afya nchini kushirikiana na Mpango wa taifa wa damu salama katika kukusanya damu na wasibaki wao kuwa watumiaji wa damu bila kuweka fedha au jitihada zozote za ukusanyaji.
Waziri Ummy amesema takwimu zinaonyesha kuwa, wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani mwaka 2015 jumla ya chupa za damu 104,632 zilikusanywa, kupimwa na kusambazwa. Idadi hii imeongezeka hadi kufikia chupa 309,376 ziizokusanywa mwaka 2019 ambayo ni ongezeko la chupa 204,744 ambayo ni sawa na asilimia 195 ikilinganishwa na chupa za damu zilizokusanywa mwaka 2015.
“Tumeboresha huduma kwenye Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa kuwapitia mashine za kisasa za kupimia damu ambapo uwekezaji huo umegharimu karibu Bilioni 13. Kwa kutumia mashine hizi Mpango una uwezo wa kufanya vipimo 4000 kwa masaa 6 kutoka vipimo 1404 kwa mashine zilizokuwepo awali kabla Serikali ya Awamu ya Tano haijaingia madarakani”. Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema tendo la kuchangia damu ni jema na linalojenga utu hivyo amewashukuru wachangia damu wote nchini hususani wale wanaochangia mara kwa mara. Pia amewahamasisha wananchi ambao hawajawahi kuchangia waweze kuchangia damu angalau mara moja kwa mwaka.
Waziri Ummy ametaka Mpango wa damu salama nchini kuweka utaratibu wa kufikia kaya zote nchini na kuhamasisha angalau awepo mtu mmoja kwa kila kaya ambae atakua anachangia damu mara kwa mara ili kuweza kukidhi mahitaji ya kitaifa ya damu salama.
Mwisho Waziri Ummy ameipongeza mikoa ya Mtwara na Lindi kwa kuweka mikakati mizuri ya uchangiaji damu ambapo mgonjwa mwenye uhitaji wa damu anahudumiwa kwanza kabla ya kutafuta ndugu wa kuchangia damu.