Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wanafunzi wa kidato cha sita katika tahasusi ya PCB, wanaojiandaa na Mitihani yao itakayo anza 29 Juni,2020 nchi nzima. **********************************
Na .Atley Kuni, MANYARA
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -TAMISEMI anayeshughulikia Afya Daktari Dorothy Gwajima akiwa na jopo la wataalam wako kwenye ziara ya siku tatu katika Mkoa wa Manyara kwa lengo la kufatilia utekelezaji wa Kanuni za Afya kwenye mashule, vyuoni na jamii kwa ujumla kama ilivyoelekezwa kwenye Miongozo ya Wizara ya Afya ikiwemo ya kujilinda na Ugonjwa wa Homa Kali ya Mafua ya Covid 19.
Akiwa katika Ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu amekagua ni mara ngapi maafisa afya na wataalamu wengine wamekuwa wakifika katika taasisi mbalimbali kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miongozo husika.
Aidha, amewataka Maafisa hao Nchi nzima kuhakikisha wanaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miongozo husika na kuhakikisha ipo kwenye taasisi zote ikiwa inafikika kwa urahisi na jamii nzima.
Akizungumza na wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Nangwa, Naibu Katibu Mkuu ameendelea kuwaasa Watumishi pamoja na Wanafunzi hao kuendelea kutembea kwenye maono makubwa ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ya kuachana na hofu na vitisho na kusonga mbele kwenye utekelezaji wa majukumu ya maendeleo ikiwemo kujiandaa na mtihani wa kidato cha sita huku wakichukua tahadhari zote muhimu zilizoshauriwa na wataalamu wa afya.
“Nataka niwaambie kwamba ugonjwa wa corona umeshadhibitiwa hivyo toeni hofu kabisa ili tuutokomeze jumla”.
Amesema, tuendelee kuvaa maono makubwa ya Mhe Rais wetu na hakika tutatokomeza hii corona pamoja na magonjwa mengine yote yatokanayo na kutozingatia kanuni za afya kama kipindupindu na kuharisha kutokanako na kula vitu vichafu kupitia mikono isiyo safi”
Amesema, Mhe. Rais katufundisha kuwa wabunifu, majasiri na kujiamini katika kupambana na adui afya na siyo kutumia mbinu zilezile miaka yote bila kujiongeza. Hivyo tujiamini kuwa tunaweza na tumeweza na tutaendelea kuweza daima.
Dkt. Gwajima amempongeza Mkuu wa Shule hiyo pamoja na uongozi wote wa Halmashauri chini ya Mkuu wa Wilaya Mhe. Joseph Mkirikiti kwa kuhakikisha wanafunzi wanapokelewa vizuri na wanaendelea kuwa na afya njema wakiwa na furaha tele na bila hofu yoyote huku wakichapa kazi ya kusoma na kujiandaa na mitihani yao tarehe 29 Juni 2020.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Manyara Bw. Samson Alute Hango, amewahakikishia wanafunzi kuwa shule hiyo ya Nangwa iliyopo Wilayani Hanang kwa sasa inao walimu wakutosha kwa masomo ya Sayansi na ukarabati mkubwa wa miundombinu kumeifanya shule hiyo kuwa na mazingira bora yakujisomea na kujifunzia.
Awali akitoa taarifa ya shule hiyo Mkuu wa shule ya Nangwa Bibi Malongo, alisema walipokea kiasi cha fedha milioni 196 katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/18 na kisha kupokea milioni 562 mwaka wa fedha 2018/19 na zote hizo zilikuwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule hii kongwe iliyopata kuwekewa jiwe la msingi na Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere mwaka 1976.
“Kwakweli tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada hizi kwani haya yote yametokea katika kipindi chake pamoja na mimi kuhamia hapa toka mwaka 2009.” alisema Bibi Malongo.
Naibu Katibu Mkuu akiwa na ujumbe wake akiwa shule ya wasichana ya Kidato cha Sita Nangwa amekagua miundombinu ya mabweni, Bwalo la chakula linaloendelea kukarabatiwa, vyumba vya madarasa, mfumo wa maji pamoja na maabara ya fizikia katika shule hiyo.
Aidha, ukarabati wa shule Kongwe nchini ni mpango endelevu unaoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya tano shabaha ikiwa ni kuhakikisha mazingira ya kufundisha na kufundishia yanakuwa rafiki kwa wanafunzi.