Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi kwenye wilaya ya Tarime mkoani Mara jana alipokuwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhandisi Mtemi Msafiri na kushoto kwa Naibu Waziri ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Mara Jerome Kiwia.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi kwenye wilaya ya Musoma mkoa wa Mara jana alipokuwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Wa pili kulia ni Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Mara Jeswald Majuva na Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Mara Jerome Kiwia.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akishangaa utunzaji Nyaraka na Majalada ya Ardhi kwenye ofisi za Ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoa wa Mara alipokuwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoka kwenye Ofisi za Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Tarime alipokuwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Mara jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Katikati) na Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Mara Jerome Kiwia wakipokea msaada wa Printer kutoka kwa Meneja wa Benki ya Posta mkoa wa Mara Agai Gilbert (kulia) wakati Benki hiyo ilipotoa msaada wa Computer moja na Printer kwa Ofisi ya Ardhi mkoa wa Mara jana ili kusaidia utekelezaji majukumu ya ofisi hiyo (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).
………………………………………………………………………………………..
Na Munir Shemweta, WANMM TARIME
Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameziagiza halmashauri nchini kufanya operesheni maalum ya kupima na kumilikisha ardhi ili kuwawezesha wananchi kuwa na hati miliki kwenye maeneo wanayoyamiliki.
Dkt Mabula alitoa maagizo hayo jana kwa nyakati tofauti katika wilaya za Tarime na Musoma mkoani Mara alipokutana na uongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi wa wilaya hizo wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoani humo.
Alisema, ni lazima halmashauri zifanye opresheni maalum ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi ili kuwawezesha wananchi kuwa na hati miliki zitakazowawezesha kuzitumia kwenye sughuli za kimaendeleo na wakati huo kuiwezesha serikali kukusanya mapato kupitia kodi ya pango la ardhi.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula, pamoja na wizara ya Ardhi katika Bajeti yake ijayo ya 2020/2021 kuwa na mpango wa kupima kila kipande cha ardhi kupitia miradi ya Benki ya Dunia na Benki ya Exim-Korea lakini halmashauri zina wajibu kuhakikisha ardhi inapimwa na kumilikishwa.
Alizitaka halmashauri za wilaya na zile za miji kutenga bajeti kwa ajili ya kazi ya kupanga na kupima maeneo na kusisitiza kuwa, zoezi hilo lisiishie katika upimaji pekee bali lifikie hatua ya umilikishaji ardhi kwa kuwapatia wananchi hati.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, vifaa kwa ajili ya kazi za upimaji vipo kwenye baadhi ya Ofisi za Ardhi za Mikoa na kuongeza kuwa kinachotakiwa ni halmashauri kuwasiliana na ofisi hizo ili kuvitumia kwenye kazi ya upimaji.
Alisema, kwa halmashauri zenye wataalam wachache wa sekta ya ardhi zinaweza kuazima wataalam kutoka maeneo mengine ikiwemo Ofisi za Ardhi za Mikoa na kubainisha kuwa kinachotakiwa ni wakurugenzi kutenga pesa ya kujikimu kwa wataalam watakaofanya kazi ya upimaji.
‘’Mnaweza kuazima wataalam kutoka maeneo mengine kama ile vofisi za ardhi za mikoa na cha msingi hapa ni kwa Mkurugenzi kutenga fedha za kuwalipa wataalam watakaoenda kufanya kazi’’ alisema Dkt Mabula.
Akigeukia suala la migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali, Dkt Mabula amezitaka halmashauri kushirikiana na ofisi za ardhi za mikoa zilizoanzishwa hivi karibuni ili kuatua migogoro ya ardhi kwenye maenro yao na kubainisha kuwa ofisi za ardhi za mikoa zisipotumika ipasavyo basi itakuwa haina maana kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhandisi Mtemi Msafiri aliipongeza Wizara ya Ardhi kwa hatua inazochukua katika kushughulikia migogoro ya ardhi nchini ambapo aliiomba ofisi ya Kamishna wa Ardhi mkoa wa Mara kuyachukua matatizo ya ardhi ya wilaya yake na kuyafanyia kazi ili kuleta suluhu miongoni mwa wananchi wenye migogoro.