………………………………………………………………………
MKUU wa Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, Joseph Mkirikiti amewataka maofisa Tarafa wa eneo hilo kutumia pikipiki walizopewa na Rais John Magufuli kuhudumia jamii kwa kuwafuata walipo kwani hivi sasa wana usafiri.
Maofisa tarafa hao watano waliopatiwa pikipiki hizo ni wa tarafa za Katesh, Simbay, Balang’dalalu, Endasak na Bassotu.
Mkirikiti aliyasema hayo juzi mji mdogo wa Katesh wakati akikabidhi pikipiki kwa maofisa tarafa watano wa eneo hilo waliopewa usafiri na Rais Magufuli.
Alisema maofisa tarafa hao wanatakiwa kutumia pikipiki hizo kwa kufikia jamii za eneo hilo ili kujua na kutatua changamoto zao ambazo zipo chini ya uwezo wao na siyo kukaa ofisini na kuwasubiri.
“Tunamshukuru Rais Magufuli kwani aliahidi na kutekeleza ahadi aliyowapa maofisa tarafa wote nchini alipokutana nao Ikulu jijini Dar es salaam mwaka jana kuwa atawanunulia pikipiki,” alisema Mkirikiti.
Aliwasihi maofisa tarafa hao kutokutumia pikipiki hizo kwa mambo mengine tofauti ikiwemo kufanyia biashara ya kubeba abiria kinyume na malengo ya serikali ya kutoa pikipiki hizo.
“Itakuwa jambo la kusikitisha kuona ofisa tarafa anatumia pikipiki hizi kubeba abiria pia muwe na tahadhari msisababishe ajali kwa uzembe,” alisema Mkirikiti.
Ofisa tarafa ya Simbay, Pius Malamsha alisema pikipiki hizo zitawasaidia kuwafikia wananchi waliopo pembezoni mwa maeneo yao tofauti na awali kabla hawajapata usafiri.
Malamsha alisema hivi sasa wataweza kufikia wananchi kwa urahisi hasa maeneo ya pembezoni ikiwemo vijiji vya kata za Gisambalang ambavyo vimepakana na wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
“Awali tulikuwa na changamoto ya usafiri hivyo kuwa na wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku tofauti na hapo mwanzo kabla ya kupata usafiri huu,” alisema.