********************************
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainab Kawawa amewataka wafanyabiashara kuacha kususia kutumia Bandari ya Bagamoyo na kuwasihi waendelee kuingiza bidhaa zao na kusafirisha bidhaa zinazotoka nje ya Bagamoyo kwani kususia kwao inasababisha hasara kwa serikali.
Aidha Kawawa amemuagiza Meneja Bandari ya Bagamoyo ,Witharo Jared Witharo kuacha mara moja vitendo anavyoshutumiwa navyo vya ukiukwaji wa maadili, kanuni, sheria na taratibu za Utumishi wa umma na ahakikishe anatoa huduma bora ili kurejesha hadhi ya bandari hiyo kama ilivyokuwa mwanzo.
Tuhuma hizo zimesababisha mtikisiko mkubwa wa kimapato baada ya mapato yanayotokana na bandari kushuka kutoka Shilingi Bilioni 03 Mwezi Novemba Mwaka 2019 hadi kufikia Shilingi Milioni 293.8 Mwezi Mei mwaka huu baada ya wafanyabiashara hao kususia kuingiza mizigo kupitia bandari hiyo.
Aliyasema hayo alipofanya mkutano maalum na wafanyabiashara wa Bagamoyo wanaotumia bandari ndogo ya Bagamoyo baada ya wafanya biashara hao kuacha kutumia bandari hiyo wakidai huduma zisizoridhisha toka kwa uongozi wa mamlaka ya bandari ya Bagamoyo.
Akizungumza kwa niaba ya Wafanyabiashara wanaotumia bandari ya Bagamoyo, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara hao ,Shabani Khamsini Almaarufu “Chavurugu” alisema, Uongozi wa Mamlaka ya bandari ya Bagamoyo umekuwa ni kero kwa wafanyabiashara kwani baadhi ya Maofisa Bandari wamekuwa na lugha chafu za matusi kwa wafanyabiashara hao, kutoa risiti zenye kiwango tofauti na pesa wanazolipia huduma.
Wakati mwingine kutishia kuwapiga wanapofika Ofisi za bandari kupata ufafanuzi na huduma, Anasema Mwenyekiti huyo.
Baada ya kupokea kero na malalamiko ya wafanyabiashara hao Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo alieleza, ni kinyume cha kanuni, taratibu, sheria na miongozo ya Utumishi wa umma kwa mtumishi kutoa lugha chafu kwa wateja anaowahudumia, kuwapiga na kuhujumu mapato ya serikali kwa kutoa risiti inayotofautiana na kiasi cha fedha alichopokea.
Kawawa aliwataka wafanyabiashara hao kuhakikisha tuhuma walizowasilisha kwake zina ukweli kwani mara baada ya mkutano huo kamati ya Ulinzi na usalama itaanza uchunguzi wa tuhuma hizo mara moja ili sheria ichukue mkondo wake kwa maofisa wote wanaohusika na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa umma, maana vitendo hivyo vimeiingizia Serikali hasara kubwa baada ya wafanya biashara hao kuisusa bandari ya Bagamoyo na kuacha kabisa kuingiza bidhaa kupitia bandari ya Bagamoyo.
“Naombeni rudini itumieni bandari ya Bagamoyo, ni mali yenu, ni kwa ajili yenu, chonde chonde rudini mtumie bandari yenu kibiashara, nipo pamoja nanyi kusimamia haki zenu na maslahi yenu na nawaahidi kufuatilia na kumaliza kero na malalamiko yenu yote na wote wanaohusika katika kuwakwamisha ntahakikisha wanachukuliwa hatua stahiki,”