Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji Damu wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Dkt. Avelina Mgasa.
……………………………………………………………………………………………………
MPANGO wa Taifa wa Damu Salama ulio chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto umetoa rai kwa Wananchi kutoa taarifa kwa wanaouza damu ili wachukuliwe hatua kali za kisheria kwani damu inatolewa bure kwa wahitaji.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji Damu wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Dk. Avelina Mgasa wakati wa Semina iliyofanyika kwa njia ya mtandao na kushirikisha Waandishi wa habari za Afya zaidi ya 30 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya siku ya Wachangiaji damu Duniani hapo Juni 14.
Dkt.Mgasa alisisitiza juu ya Wananchi kuripoti endapo watakutana na vitendo hivyo vya kuombwa pesa ili kupatiwa damu kwani tayari sheria zimeanza kuchukuliwa kwa watendaji wasio waaminifu.
“Wananchi wasiogope kusema. Tanzania bado hatujaanza kuuza damu.
Damu ni bure kama watakutana na vitendo vya kuombwa pesa basi waripoti kwa Mganga mkuu wa kituo, Hospitali husika.
Kwa sasa tunao mfano mzuri kwa hatua zilizochukuliwa ikiwemo kule Wilaya ya Kongwa”. Alisema Dkt. Mgasa.
Aidha, Dkt. Mgasa alitoa wito kwa watoa huduma kwa Mgonjwa anapohitaji damu na kama ipo apewe.
“Hatuwezi kuacha mtu apoteze maisha kwa kukosa damu.
Ndio maama tunahamasisha watu kuchangia damu kwa hiyari ili kuokoa ndugu ama jamaa zetu watakapata tatizo” alisema Dk. Mgasa.
Aidha, akiwasilisha mada kwa kina namna ya Mpango wa Taifa wa damu salama;
Alisema kuwa kutokana na janga la mlipuko wa virusi vya corona (COVID-19) nchini, kiwango cha uchangiaji damu kimeshuka kutoka chupa 31,502 za mwezi Februari, chupa 25,737 za mwezi Machi hadi kufikia chupa 22,044 Mwezi Aprili.
“Hali hiyo imechangiwa na shule na vyuo kufungwa hivyo kukosa fursa za kukusanya damu katika ofisi mbalimbali.
“Kingine ambacho kimesababisha ukasanyaji wa damu kuwa mdogo ni zuio la mikusanyiko kutokana na maelekezo ya Serikali katika kupambana na Covid-19 kwani maeneo hayo ndiyo yamekuwa yakitegemewa zaidi”. Alisema Dk. Mgasa.
Dk Mgasa amesema kwa sasa wamejipanga katika kuhakikisha watu wanachangia damu katika mazingira salama ambayo yatawawezesha kujikinga na Covid-19.
“Kutokana na hilo basi uhitaji wa damu ni mkubwa sisi kama damu salama tumejipanga kwani uchangia wa damu ni tendo salama na mpango umeweka mikakati mbalimbali ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Corona katika vituo vya kuchangia damu.
“Tumuweka maji tiririka na sabuni kwaajili ya kunawa mikono, Vitakasa mikono, Vifaa kinga kwa watumishi kama barakoa, apron/koti, gloves, na goggles, Thermo scanner kwa ajili ya kupima jotoridi la mwili kwa kila mchangia damu.
“Tunatakasa vitanda na vifaa vinavyotumika na wachangia damu, mpangilio unaozingatia umbali kati ya mtu na mtu (social distance)”. Alieleza Dk Mgasa.
Katika maadhimisho ya mwaka huu Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu anatarajiwa kuongea na Wananchi na kuwashukuru wachangia damu.
Dk. Mgasa alisema kampeni kwa mwaka huu yenye Kaulimbiu katika maadhimisho hayo ni “Damu Salama Inaokoa Maisha”- (“Safe Blood Saves Lives”) ikiwa na malengo ya kukusanya chupa za damu 24,800.
Dk. Mgasa alimalizia kwa kutoa wito kwa wachangia damu kukitokeza kwa wingi kuchangia kwa hiyari kwenye maeneo yote ya Kanda hapa Nchini huku kwa Kanda ya Mashariki ikiwemo Dar es salaam yenye vituo 10 ndio yenye uhitaji mkubwa zaidi.
“Mahitaji ya damu ni makubwa zaidi kanda ya Mashariki.
Chupa nyingi za damu zinahitajika na zinatumika kwa wingi ikiwemo Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, taasisi ya Mifupa (MOI) na maeneo kwingine”. Alisema.
Alivitaja vituo hivyo vya kuchangia damu ni pamoja na:
Ofisi zote za Kanda za mpango wa Taifa wa Damu Salama, Hospitali zote za Rufaa za Mkoa, Hospitali za zote Halmashauri nchini.
“Kwa Dar es Salaam tuna vituo 10 ambavyo ni Hospitali za Rufaa za Mkoa Amana,Mwananyamala na Temeke.
Zipo pia Hospitali ya Jeshi Lugalo, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Mbweni, Vijibweni na Mbagala Rangi Tatu” alisema Dkt. Mgasa.
Akimalizia katika mafunzo hayo, alibainisha kuwa zoezo la utoaji damu ni umakini na hivyo amewatoa hofu wananchi hasa kipindi ambacho dunia inaendelea kuoambana na COVID-19.
“Kabla ya kuchukua damu unadodoso utapitia. Na tutakushauri.
Suala la mtu aliyeumwa Corona anaweza kuchangia damu endapo atathibitishwa amepona.
Kw sasa haijathibitika kitaalam kama Corona inaambukizwa kwa njia ya damu.
Mpango wa taifa qa damu salama tunashauri aliyeumwa mfano Typhoid anatakiwa achangie damu baada ya kupita miezi sita (6) lakini pia kwa mwaanamke aliyeingia Headhi anapoteza damu nyingi inapendeza achangie kila miezi minne” alisema Dkt. Mgasa.
Aidha, aliwashukuru Wananchi kuendelea kujitolea damu ambapo zimekuwa msaada mkubwa wa kuokoa maisha ya watu.