**********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Rais mstaafu Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ameushukuru uongozi wa chuo Kikuu cha Dar es Salaam kukamilisha utaratibu kuhakikisha hosteli za Magufuli kuwa salama kabla ya wanafunzi kufika Chuoni hapo Juni 1 mwaka huu.
Akizungumza baada ya kutembelea hosteli hizo Dkt.Kikwete amesema kuwa wasingependa kama hosteli hizo zikawa ni chanzo cha maambukizi ya magonjwa na kusambaa hivyo amehakikishiwa kuwa hosteli hizo ni salama hivyo wanafunzi wanatakiwa wafike bila wasi wasi.
“Makubaliano yetu wale tuliowakabidhi hosteli hizi kwaajili ya usalama wafanye usafi na wamefanya na majibu waliotuletea ni kwamba pako salama hivyo nawahakikishia vijana pako salama njooni mkae wale tuliowakabidhi wameshafanya vile mbavyo tulikubaliana”. Amesema Dkt.Kikwete.
Nae Bi.Neema Kweba ambaye alifika kwa niaba ya Mgaga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesema kuwa wao kama timu ya afya walianza kutumia majengo hayo kuanzia Aprili 5 mpaka Aprili 25 majengo haya yalitumika kwaajili ya kutunza wasafiri ambao waliingia hapa nchini kuwaweka kwaajili ya sababu za kiusalama zaidi
Amesema wakiwa katika majengo hayo waliendelea kuzingatia mambo yote ya muhimu ya kiafya katika kujikinga na kuwakinga wale waliokuwa wanawahudumia kutokana na ugonjwa wa Corona.
“Mpaka tunaondoka hapakuwa na kesi yoyote ya mtu wa Corona iliyotoka katika hosteli hizi za Magufuli lakini mara baada ya watu kuanza kuondoka Aprili 25 tulianza utaratibu wa usafi na majengo yote yalifanyiwa usafi kwa maana ya utakasaji na mpaka kufikia Mei 25 shughuli hiyo ilikuwa tayari imeshasha”.Bi.Neema
Hata hivyo Bi.Neema amesema kuwa takataka zote zilizotengenezwa kipindi watu walikuwa katika hosteli hizo zimeshaondolewa.
Bi.Neema amesema kuwa baada ya kuondoka katika hosteli hizo wameacha vivaa kama vile matanki kwaajili ya kusafisha mikono pamoja na kichomea taka ambavyo vitasaidia wanafunzi kuendelea kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa William Anangisye amesema kuwa kufuatia tangazo la kufunguliwa kwa vyuo, Chuo hicho kimefanya maandalizi ya kutosha kuwakaribisha wanafunzi wa chuo hicho.
“Kila mwanafunzi atatakiwa kuvaa barakoa na tutajitahidi kuhakikisha kila mwanafunzi awe na kitakasa mikono kwaajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona”.Prof.Anangisye.