- Wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini kunufaika na utoaji wa elimu bure kupitia jukwaa la kidijitali.
- Shule za msingi na sekondari kunufaika na upatikanaji bure wa maudhui ya elimu kupitia jukwaa la ‘Vodacom Instant Schools portal’.
25 Mei 2020, Dar es Salaam. Kampuni inayoongoza kidijitali nchini ya Vodacom Tanzania PLC inafanya kazi na shule pamoja na taasisi mbalimbali za elimu nchini kutoa huduma ya mafunzo ya dijitali bila gharama yoyote. Taasisi zilizonufaika na huduma hii ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mkolani Foundation Health Sciences Training Institute, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yosefu (SJUIT), College of Health and Allied Sciences na Shule Direct kwa uchache; ili kuwasaida wanafunzi kupata elimu bure kidijitali.
Ni wazi kuwa ufundishaji na kusoma kupitia mtandao, mikutano na vikao vinavyofanyika kupitia mtandao, burudani za nyumbani na ufanyaji kazi nje ya ofisi inakuwa mfumo mpya duniani. Hali kadhalika, data ndio ufunguo wa kusaidia biashara na elimu kuendelea pamoja na kuwezesha sehemu zingine katika jamii kuendelea kuwasiliana ikiwemo kati ya mtu na mtu, au watu na wapendwa wao.
Huduma hii ya kutotoza gharama yeyote kwa Taasisi za elimu zinazofundisha kupitia mtandao inasaidia moja kwa moja shule za msingi na sekondari, wanafunzi wa elimu ya juu, walimu, wahadhiri na wazazi kote nchini. Taarifa hii imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania PLC ambaye pia ni mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Bi. Rosalynn Mworia.
‘‘Tunaunganisha watanzania kwa matendo mema kupitia mtandao SUPA wa Vodacom ambao unapatikana nchini nzima, tunataka kuwasaidia Watanzania kwa kuwaunganisha na hivyo kuwasaidia kufanya kazi kwa tija popote walipo. Kupitia ofa hii ya kipekee, Vodacom inashirikiana na taasisi mbalimbali za elimu kuwawezesha wanafunzi waliopo shule za msingi, sekondari na elimu ya juu kujisomea kupitia jukwaa la bure la elimu katika mtandao SUPA,’’ alisema Mworia
Aliongeza kuwa, ‘Tunaendelea kuona hamasa toka kwa wabunifu nchini kote ambao wanaendelea kutufikia wakiomba kushirikiana nasi. Hii inatia moyo kwa sababu jamii ya kitanzania inatutaka kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha watoto wetu wanaendelea kujifunza bila kujali kwamba shule zimefungwa kwa muda.’’
Kwa miaka mingi, kampuni ya Vodacom Tanzania PLC imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha upatikanaji wa elimu bora kupitia mifumo ya kidijitali – kwa kuamini kwamba teknolojia inaleta mapinduzi kupitia muunganisho unaoleta fursa kwa kila mtu ili wafikie uwezo na kupata maarifa kamili.
Awali, Vodacom wameshirikiana na wadau mbalimbali kama Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini (UCSAF), Taasisi ya Tanzania Data Lab (Dlab) na kampuni ya Samsung ili kuchochea mafunzo ya dijitali nchini.
Kwa kuongezea, wateja wote wa Vodacom na wale wasiokuwa wateja wanaweza kufurahia upatikanaji bure wa elimu kupitia Vodacom Instant Schools – jukwaa la bure la elimu mtandaoni, inayotoa maudhui ya kujifunza kidijitali kwa wanafunzi na walimu kupitia simu za mkononi na kompyuta. Maudhui haya yanapatikana kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari bure, unachohitaji ni laini ya Vodacom.
‘‘Vodacom imejidhatiti kuendelea kutoa msaada kwa wateja wake na Watanzania kwa njia yoyote tutakayoweza, wakati huu tukiendelea kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa huu wa CORONA,’’ alimalizia Mworia.Kuhusu Vodacom Tanzania:
Vodacom Tanzania PLC ni watoa huduma ya mawasiliano ya simu za mkononi wanaoongoza wenye mtandao wa data wenye kasi zaidi nchini. Tunatoa huduma za mawasiliano kwa zaidi ya wateja milioni 15. Kampuni ya Vodacom Tanzania pamoja na kampuni zake tanzu ni sehemu ya Kundi la makampuni ya Vodacom (Vodacom Group) iliyosajiliwa Afrika Kusini ambayo kwa upande mwingine inamilikiwa na kundi la makampuni la Vodacom Plc la Uingereza. Kampuni ya Vodacom imesajiliwa katika soko la hisa la Dar es salaam (DSE) kwa namba ISIN: TZ1886102715 Stock name: VODA.
Kwa maelezo zaidi tafadhali tembelea tovuti yetu ya: www.vodacom.co.tz