………………………………………………………..
Na Mwandishi Maalum Dodoma
Watanzania leo (22/05/2020) wanaanza maombi ya kitaifa kwa siku tatu mfululizo kila mmoja kwa imani yake ili kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua iliyofikiwa katika mapambano dhidi ya Janga la Corona.
Maombi hayo ya siku tatu, (Ijumaa, Jumamosi na Jumapili (Tarehe 22-24 Mei, 2020) yanafuatia wito wa Rais John Magufuli kupitia Hotuba yake aliyoitoa Jumapili ya tarehe 17 Mei, 2020 wakati akitoa takwimu za Corona katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Rais Magufuli aliwahimiza Wananchi katika kipindi hiki cha Siku tatu za kumshukuru Mwenyezi Mungu kuendelea kufuata maelekezo ya Wataalam wa afya na kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka, kuepuka misongamano isiyo ya lazima na kuvaa Barakoa.
Alisema maombi ya kitaifa ni kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kujibu maombi ya Watanzania yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 17-19 Aprili 2020.
Aliwahimiza Viongozi wa madhehebu yote ya dini kuongoza maombi na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kupungua maambukizi ya Virusi vya Corona, ujumbe ambao amesisitiza juzi wakati akizungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali Mkoani Singida.
Makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo viongozi wa dini wamepongeza hatua ya Rais Magufuli wakisema hotuba yake imewapa matumaini mapya katika mapambano dhidi ya Janga la Corona.
JIKINGE, WAKINGE WENGINE CORONA INAZUILIKA.