UTEKELEZAJI wa miradi ya miundombinu mbalimbali ikiwemo nishati, reli, maji, barabara, na viwanja vya ndege ni miongoni mwa viashiria muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa lolote duniani.
Tanzania imedhamiria kukuza uchumi wake na kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda. Ili lengo hilo liweze kufanikiwa ni lazima iwe na miundombinu bora na imara.
Katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imejikita kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati itakayowezesha lengo hilo kufikiwa.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), lengo likiwa ni kupunguza gharama, muda wa kusafiri na kuimarisha shughuli za biashara kati ya Tanzania na nchi za jirani.
Mradi mwingine mkubwa wa kimkakati unaotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano ni ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unaotekelezwa katika maporomoko ya bonde la Mto Rufiji.
Mradi huo, unatarajiwa kuzalisha umeme wa kutosha utakaosaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini sambamba na kuiwezesha Serikali kutekeleza kwa kasi Sera ya Viwanda.
Vilevile, mradi huo wa JNHPP ambao ujenzi wake unaendelea kwa kasi, utakapokamilika utazalisha umeme wa megawati 2,115 zitakazoingizwa kwenye gridi ya Taifa ili kuongeza chachu ya maendeleo ya wananchi.
Katika kuhakikisha miradi hiyo muhimu itakayochangia kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa kati inakamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa, Alhamisi ya Mei 14 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea miradi hiyo ili kukagua maendeleo yake.
Waziri Mkuu alianza kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere ambapo alisema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo mkubwa na wa kimkakati.
Aliongeza kuwa kazi inayofanyika ni ya uhakika na kwamba kuna matumaini makubwa ya kukamilika mapema kwa mradi huo kabla ya muda uliopangwa. Mradi huo ulianza kutekelezwa Juni 14, 2019 na unatarajiwa kukamilika Juni, 2022.
Licha ya ujenzi huo kuendelea vizuri, Waziri Mkuu alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka asimamie mradi huo ili ukamilike kwa wakati.
“Nimetembelea eneo la mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji unaojengwa na kampuni ya Arab Contractors kwa pamoja na kampuni ya Elsewedy Electric zote za kutoka nchini Misri na nimeridhishwa na hatua iliyofikiwa”. Alisisitiza Waziri Mkuu.
Kadhalika, Waziri Mkuu alimwagiza mkandarasi anayejenga mradi huo aukamilishe kwa wakati kwa sababu imebainika kuwa mvua zinazoendelea kunyesha nchini haziathiri utekelezaji wa ujenzi huo.
Mbali na kuliwezesha Taifa kuwa na umeme wa uhakika, pia mradi huo utawezesha kupungua kwa changamoto ya ajira baada ya Watanzania wengi wakiwemo wakandarasi kupata ajira za kudumu na za muda mfupi.
Kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo, kutaiwezesha Tanzania kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kitakachosaidia kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwamo mradi wa reli ya kisasa pamoja na kusaidia kukuza uchumi wa viwanda.
Hafla ya utiaji saini ya Mkataba wa Ujenzi wa Mradi huo ilifanyika jijini Dar es Salaam, tarehe 12 Desemba, 2018 na kushuhudiwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu wa Misri Dkt. Mostafa Madbouly.
Pia, mradi huo utapanua wigo wa vivutio vya utalii nchini kama uanzishwaji wa safari za boti kupitia bwawa kuu yaani utalii wa uvuvi, hivyo kubadilisha maisha ya wakazi wanaoishi ndani na nje ya eneo la mradi.
Baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa kuzalisha umeme wa JNHPP, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na kusema kuwa miradi hii imesaidia kupungua tatizo la ajira kwa kuajiri wafanyakazi 18,700.
“Kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huu, kumesaidia kupunguza ukosefu wa ajira kwa kutoa ajira 7,400 kwa kipande cha Dar hadi Morogoro. Kipande cha Morogoro hadi Makutopora, Singida kimetoa ajira 6,300 wakati mradi wa umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere nao pia umetoa ajira 5,000.”
Waziri Mkuu amesema hayo baada ya kutembelea mradi huo na kuzungumza na wananchi aliowakuta kwenye stesheni ya Soga, iliyoko wilayani Kibaha, mkoani Pwani.
Alisema faida nyingine ya mradi huo katika awamu yake ya kwanza, ni kupunguzwa kwa muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Morogoro, ambapo aliwataka wananchi hao waulinde mradi huo kwa sababu utakapokamilika utawanufaisha na wao pia.
Reli hiyo itakuwa na vituo sita vya Dar es Salaam, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere na Morogoro, huku vituo vya Dar es Salaam na Morogoro vikiwa ndiyo vituo vikuu. “Kwenye vituo vya kushusha abiria vya reli hii, kutakuwa na huduma za kibenki na maduka, kwa hiyo wananchi hata kama hamsafiri, mtaweza kupata huduma na mahitaji yenu kutokea hapo,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Akielezea maendeleo ya mradi huo unaojengwa kwa awamu mbili, Waziri Mkuu alisema Serikali iliweka malengo ya kukamilisha mradi huo kwa wakati na ndiyo maana aliamua kwenda kuukagua.
“Katika awamu ya kwanza, ambayo inatoka Dar es Salaam hadi Morogoro (km. 300), mradi huu umekamilika kwa asilimia 77.91. Hii maana yake ni kwamba wamemaliza kazi hii kwa zaidi ya robo tatu. Wametengeneza njia na kulaza mataruma na mimi nimekuja na hii treni maalum kwa karibu kilometa 20.”
“Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli alianzisha mradi huu na kuwaahidi Watanzania kwamba tunaweza kuujenga kwa fedha zetu. Vilevile, mradi huu ni utekelezaji wa agizo la Ilani ya CCM ambalo linaitaka Serikali ya awamu ya tano iimarishe usafiri wa reli nchini.”
Alisema katika kutekeleza agizo hilo, Serikali ya awamu ya tano, mbali ya kujenga reli hiyo ya kisasa, imefanikiwa pia kufufua reli ya kutoka Dar – Tanga – Moshi ambayo ilikuwa haitumiki kwa zaidi ya miaka 20. Huduma ya mizigo katika reli hiyo ilikuwa haifanyi kazi kwa miaka 12 na huduma ya kusafirisha abiria ilisitishwa tangu mwaka 1994.
Akielezea kuhusu awamu ya pili ya ujenzi wa mradi huo, Waziri Mkuu alisema ujenzi wa reli kutoka Morogoro hadi Makutupora, Singida (km. 422) ulianza mwaka jana mwishoni na sasa hivi umefikia asilimia 30 ya kazi, ambapo wanatarajia kuukamilisha ifikapo Juni, 2021.
Waziri Mkuu alisema sambamba na ujenzi wa reli hiyo, umeme pia umeanza kuwekwa ambapo nguzo 154 kati ya 160 zinazotakiwa kuwepo zimeshasimikwa. “Tumeweka miundombinu ya umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere, kutoka Kidatu na Kinyerezi. Nia yetu ya kupata umeme kutoka vyanzo vyote vitatu, ni kuhakikisha kuwa umeme upo saa zote.”
“Tuna uhakika wa kutumia umeme wa Kinyerezi na Kidatu au Kidatu na Mwalimu Nyerere au Mwalimu Nyerere na Kinyerezi hata umeme ukikatika kabisa, mabehewa yetu yana uwezo wa kutunza umeme kwa dakika 45, na katika muda huo, ni lazima tutakuwa tumerejesha umeme kutoka chanzo kimojawapo.”
Waziri Mkuu alisema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa reli hiyo na akawapongeza mafundi wa kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki ambayo inajenga reli hiyo. “Kampuni ya Yapi Merkezi imefanya kazi kama walivyosaini kwenye mkataba na Serikali na ninaamini watakamilisha kazi kabla ya muda.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye, alisema kuwa lengo la ziara hiyo ya Waziri Mkuu ni kuangalia maendeleo ya mradi huo na utayari wake wa kuanza kazi katika kipindi cha miezi miwili ijayo.
Naibu Waziri huyo alisema kuna vituo vidogo vilibakia ambavyo ujenzi wake ulisimama kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini.
Alisema reli hiyo ya kisasa itakapokamilika wananchi watafanya safari kwa haraka na ambapo kutoka Dar es Salam hadi Morogoro itakuwa kwa muda wa saa 1.30. Aliongeza kuwa treni hiyo ya kisasa ina faida kiusalama kwani kila itakapokuwa inatembea inajulikana maeneo yote inayopitia.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa alisema gharama ya ujenzi wa mradi huo wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salam hadi Makutopora Singida utagharimu kiasi cha sh trilion saba hadi kukamilika.
Mkurugenzi Kadogosa alisema hadi sasa ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salam hadi Morogoro kwa urefu wa kilomita 300 umekamilika kwa asilimia 77.9. Alisema mvua zinazoendelea kunyesha zilisababisha baadhi ya kazi kutokamilika kwa wakati.
Awali, Meneja Mradi Msaidizi, Mhandisi Ayoub Mdachi alisema treni ya mizigo itakuwa na uwezo wa kubeba tani 10,000 kwa mara moja na itatembea kilometa 120 kwa saa huku treni ya abiria ikitembea kilomita 160 kwa saa.