Wakulima wakivuna mpunga Wilayani Kahama kwenye majaruba yaliyo na maji.
Hali ya mpunga ukiwa katika hatua za uvunaji shambani Kijiji cha Nyanhembe Kahama.
Baadhi ya wakulima wakivuna mpunga katika Kijiji cha Chanhembe Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
…………………………………………………………………………………
Na.Mwandishi Wetu.
WAKULIMA wa zao la Mpunga Wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamesema kuwa huenda mazao yao yakaozea shambani kutokana na ukosefu wa barabara hali ambayo inapelekea vyombo vya usafiri kushindwa kufika katika maeneo hayo katika kipindi hiki cha mavuno.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Nyanhembe Agricultural Farm inayojishughulisha na shughuli za Kilimo na Ufugaji Khamis Mgeja alisema hayo mwanzoni mwa Juma hili alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea shamba lake la mpunga lililopo katika kijiji cha Nyanhembe Kata ya kilago halmashauri ya Mji wa Kahama Wilayani .
“Kwa kweli tuna changamoto kubwa unakuta mkulima anapakia mpunga kwenye mabega kwani hata tela la kukokotwa na ng’ombe haliwezi kupita kutokana na mvua kuzidi kwa mwaka huu na kingine ninachoomba ni maafisa ugani nao waweze kututembelea ili kuweza kuona changamoto hizi”amesema Mgeja.
Pia Mgeja aliipongeza serikali kupitia wizara ya kilimo chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wa kumkomboa mkulima kwa kutoa maelekezo ya kulielekeza shirika la Taifa la kuhifadhi chakula (NFRA) kuanza kununua mazao mbalimbali msimu huu na kuacha mazoea ya kununua zao moja tu la mahindi.
“Kwa kweli nitumie fursa hii kuipongeza serikali kwa maamuzi mazuri ya kumkomboa mkulima hasa kwa kuielekeza NFRA Kuwa na mpango kabambe wa kununua mazao mbalimbali nah ii itamwondolea mzigo mkulima hususan mzigo wa kupunjwa mazao yake pindi anapouza”amesema.
Baadhi ya wakulima katika Kijiji cha Nyanhembe Wilaya ya Kahama akiwemo Salima Kazinza na Emmanuel Masebu Walisema hali yam waka huu imekuwa tofauti na mwaka uliopita hasa katika suala la uvunaji ambapo karibu mashamba yote ya mpunga yana maji pamoja na njia za kwenda shambani hivyo wao wamekubaliana na hali na hawana jinsi huku wakibainisha kuwa mwaka huu umekuwa wa neema kwa kupata mazao mengi licha ya changamoto ya kuyasafirisha kwenda nyumbani.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Anderson Msumba alisema halmashauri imekuwa ikiwatengenezea mazingira Rafiki wakulima ikiwa ni pamoja na kuchimba mabwawa lakini changamoto iliyopo kwa sasa ni kuzidi kwa kiwango cha mvua hata kwenye kipindi cha mavuno.
Wilaya ya Kahama ni miongoni mwa Wilaya hapa nchini ambapo zao kuu la chakula na biashara ni Zao la Mpunga likifuatiwa na zao la Mahindi ambapo pia Wilaya hiyo iliyopo Mkoani Shinyanga ni maarufu kwa kilimo cha zao la tumbaku nap amba pamoja na Uchimbaji wa Madini.