Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu akisoma tamko juu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, mbele ya waandishi wa Habari hii leo Jijini Dodoma. Kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika kwa kutumia vyombo vya habari bila kuwapo kwa mikusanyiko.
……………………………………………………………………………
Na Lulu Mussa,Dodoma.
Serikali imesema kuwa mwaka huu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Kitaifa yaliyopangwa kufanyika Mkoani Lindi tarehe 5 Juni 2020 hayatafanyika kutokana na mlipuko wa Ugonjwa wa Homa ya Mapafu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan katika Mkutano wake na Waandishi wa habari uliofanyika Jijini Dodoma.
“Kama mnavyofahamu, Nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na janga la ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona. Ugonjwa huu unaambukizwa kwa njia mbalimbali ikiwemo mikusanyiko ya watu. Uwepo wa janga hili umesababisha kusitishwa kwa shughuli zinazohusu mikusanyiko ya watu wengi.” Zungu alisisitiza.
Kwa muktadha huo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wamekubaliana kuwa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatafanyika kwa kutumia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii kuelimisha na kuhamasisha jamii kutunza mazingira na kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa wa corona.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Mazingira ambao ni UNDP, UNEP, WWF, GIZ, Forum CC, Vodacom Foundation, USAID, nchi wahisani pamoja na vyombo vya habari tunahamasisha na kuelimisha jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi kwa kuhifadhi Mazingira hivyo kutakuwa na mashindano ya kuandika insha kuhusu mabadiliko ya tabianchi na mikutano ya kitaalamu itakayofanywa kwa njia ya mitandao kwa kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa wa Corona” Zungu alisema.
Waziri Zungu ameikumbusha jamii kuwa hifadhi ya mazingira si kazi ya Serikali pekee yake bali ni jukumu la kila mmoja katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kaya na ametoa wito kwa vyombo vya habari, taasisi zote za Serikali na asasi za kiraia kusaidia katika kuhifadhi mazingira.
“Watendaji wote katika ngazi zote hatuna budi kushirikiana katika kutekeleza kwa ukamilifu Sheria na Kanuni za hifadhi ya mazingira. Kila mmoja ana wajibu na fursa muhimu katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira hapa nchini. Ningependa kusisitiza kuwa tushirikiane katika kufanya jitihada mbalimbali ili kupambana na uharibifu wa mazingira kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.” Waziri Zungu alisisitiza.
Amesema kila mwananchi akiwajibika katika nafasi yake, tutalinda mazingira yetu na jamii kwa ujumla. Hivyo, shughuli za maadhimisho ya Siku ya Mazingira hapa nchini mwaka huu pamoja na mambo mengine, zitalenga kuhamasisha jamii kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuelimishana jinsi ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Kila tarehe 5 Juni, nchi yetu huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kitaifa yalipangwa kufanyika mkoani Lindi na Kauli mbiu ya maadhimisho haya kitaifa ni Tuhifadhi Mazingira: Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.