Muonekano wa Basi jipya dogo la Klabu ya mpira wa miguu ya Jeshi la Magereza(Tanzania Prisons Sport Club) lilonunuliwa kwa thamani ya Tsh. Milioni 75.
……………………………………………………………………………….
Na ASP. Lucas Mboje, Dodoma.
KATIKA kutatua changamoto ya usafiri kwa Klabu ya mpira wa miguu ya Jeshi la Magereza(Tanzania Prisons SC). Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Suleiman Mzee ameipatia Klabu hiyo Basi dogo aina ya Costa lenye thamani ya Tsh. Milioni 75 kwa ajili ya kuisafirisha Timu kwenda mikoa mbalimbali nchini.
Akizungumza katika makabidhiano ya gari hilo hivi karibuni jijini Dodoma, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Suleiman Mzee amesema kuwa kwa muda mrefu Klabu hiyo haikuwa na usafiri hivyo iliwalazimu Uongozi wa Klabu kukodi magari hivyo kuongeza gharama za uendeshaji wa Klabu.
“Nimefanya maamuzi ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto ya usafiri kwa Timu yetu na katika kupunguza gharama za kukodi magari hivyo nimewapatia Basi dogo jipya kwa ajili ya Timu ili waweze kulitumia kwenda sehemu mbalimbali nchini kwa mujibu wa ratiba za Ligi Kuu”, amesema Kamishna Jenerali Mzee.
Kwa upande wake Mkuu wa Sehemu ya Michezo, Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, SSP. Matlida Mlawa akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa Klabu hiyo amemshukru sana Kamishna Jenerali wa Magereza Suleiman Mzee kwa kutatua changamoto hiyo ya usafiri lakini pia kwa kuthamini tasnia ya michezo Jeshini.
“Nichukue nafasi ya kipekee kumshukru Kamishna Jenerali Suleiman Mzee kwa kutupatia usafiri huu na nina imani kubwa kwamba ataleta mageuzi makubwa ndani ya Jeshi la Magereza”, amesema SSP. Mlawa.
Klabu ya Jeshi la Magereza Tanzania Bara ilianzishwa mwaka 1996 na imekuwa na historia kubwa katika tasnia ya mchezo wa mpira wa miguu nchini ambapo Mwaka 1999 Timu ya Tanzania Prisons SC iliweza kuchukua ubingwa wa Ligi ya Muungano chini ya Kocha Mkuu Boniphace Mkwasa. Klabu hiyo ina makazi yake jijini Mbeya na inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara iliyosimama kufuatia uwepo wa ugonjwa wa Corona nchini – COVID19.