…………………………………………………………………….
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa Chanjo wameendesha semina maalumu kwa njia ya mtandao kwa Waandishi wa Habari zaidi ya 50 nchini.
Semina hiyo ya siku moja ya uelewa wa Chanjo ya kukinga ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi (HPV Vaccine) ambayo hutolewa bila malipo kwa wasichana wa miaka 14 hapa nchini iliendeshwa mubashara kupitia mtandao wa ZOOM.
Awali akiwasilisha mada maalumu ya chanjo hiyo ya HPV, Afisa Mradi, Mpango wa Taifa wa Chanjo-Wizara ya Afya, Bi. Lotalis Gadau alisema licha ya uwepo wa Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19) wamejipanga kuendelea kutoa huduma hiyo kwa kufuata miongozo iliyopo.
Aliwataka Wazazi kuruhusu wasichana ambao kwa sasa wapo majumbani kupatiwa chanjo hizo katika vituo vya kutolea huduma za Afya sambamba na kufuata taratibu za kujikinga na COVID 19.
“Huduma za Chanjo ziendelee kutolewa kama kawaida ili kuepuka milipuko inayoweza kujitokeza ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Kila fursa ipatikanayo itumiwe vizuri kuhakikisha huduma za chanjo zinatolewa lakini pia elimu ya afya kabla ya utoaji wa huduma za chanjo hiyo itolewe kwa muda mfupi kuzuia msongamano na watu kukaa muda mrefu kituoni” alisema Bi. Lotalis Gadau
Aliongeza kuwa, huduma za chanjo zitolewe sehemu ya wazi na yenye hewa ya kutosha huku ikizingatia umbali wa mita moja toka kwa mwingine.
“Wasichana wanaotakiwa kupata chanjo waende vituo vya kutolea huduma za afya wasisubiri kufuatwa na huduma mashuleni kama awali
Kwa sasa shule zimefungwa hivyo wataenda kupata huduma hiyo vituo vya kutolea huduma za afya na kwa wale ambao walipata dozi ya kwanza waende na kadi zao kwa ajili ya dozi ya pili. alisema Bi. Lotalis Gadau
Aidha, alitoa ushauri kwa vituo vya afya kupanga ratiba maalumu ya kutoa huduma za chanjo ili kupunguza misongamano kwa wanaopima uzito pekee waende baada ya miezi mitatu kwa kufuata miongozo kwa lengo la kupunguza maambukizi ya COVID-19.
“Kila mtu anapaswa kufuata maelekezo ya miongozo ikiwa ni pamoja na :
Kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa barakoa muda wote na Wahudumu wajikinge muda wote (wavae PPE)” Alisema.
Akielezea kwa kina juu ya chanjo hiyo ya HPV, alisema ni salama na imekidhi vigezo vyote hivyo wazazi waendelee kuhamasisha watoto wao kupatiwa ilikujikinga na magonjwa yanayosababishwa na saratani hapa nchini.
Alibainisha kuwa, Nchi za bara la Amerika, Ulaya na nyingine zilizoendelea wamekuwa wakitumia chanjo hii kwa muda mrefu na kwa Afrika, Tanzania ni nchi ya tano (5) kuanzisha chanjo hii baada ya Lesotho, Rwanda, Zambia na Uganda.
“Chanjo hii imekuwa ikitolewa katika vituo vya Serikali, binafsi na vya mashirika ya dini, mashuleni na kwenye jamii kwa njia ya kikoba.
Chanjo hii ni salama na imethibitishwa na shirika la Afya Ulimwenguni na hapa nchini imedhibitishwa na kusajiliwa na Mamlaka ya Dawa na vifaa Tiba (TMDA).
Chanjo hii hutolewa bila malipo. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhamasisha jamii umuhimu wa chanjo hii” Alisema.
Bi. Lotalis Gadau alieleza kuwa, chanjo hiyo ilianza rasmi Aprili 2018 ikiwa na lengo ya kufikia kiwango cha asilimia zaidi ya 80 huku walengwa ni wasichana waliotimiza miaka 14.
“Chanjo hii tokea tulipoanzisha, hutulewa katika utaratibu wa kawaida vituoni na mashuleni ambapo Msichana hupata dozi mbili (2) ambazo zitapishana miezi 6.
Aidha, alivitaja visababishi na vichocheo vya saratani ni pamoja na kuanza ngono mapema katika umri mdogo chini ya miaka 18, Kuzaa idadi kubwa ya watoto hasa wanawake walioanza kuzaa wakiwa na umri mdogo (chini ya miaka 18).
Pia uvutaji wa sigara au tumbaku kupita kiasi, Kuwa na wapenzi wengi au kujamiiana na mtu mwenye wapenzi wengi,
Upungufu wa kinga (HIV) na mengine mengi.
Imeelezwa kuwa, Tanzania ni nchi mojawapo barani Afrika yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani ya Mlango wa kizazi.
Kwa mujibu wa Shirika la afya ulimwenguni (WHO) linakadiria takriban akina mama wapya 7305, wanapata Saratani ya mlango wa kizazi Tanzania kila mwaka.
Wagonjwa wengi wa Saratani ya mlango wa kizazi hawapati huduma za ugunduzi mapema
“Takwimu kutoka hospitali ya Ocean Road inaonesha kwamba, Saratani ya Mlango wa Kizazi inachangia kwa asimilia 36 ya saratani zote.
Asilimia 70 ya wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi wanajitokeza katika hatua ambayo tayari saratani imesha sambaa maeneo mengine mwilini.
Pia Wakina mama walio na maambukizi ya VVU wanaathirika zaidi na saratani hii” Alimalizia Bi. Lotalis Gadau.