▪︎ Aagiza utekelezaji wa hukumu na utatuzi wa migogoro ya ardhi Ifakara

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewaonya watendaji wa Serikali wanaopuuza hukumu za mahakama na kusisitiza kuwa kiongozi au taasisi yoyote isiyoridhika na hukumu inapaswa kukata rufaa badala ya kukaidi utekelezaji wake.

Alitoa onyo hilo jana (Jumatano, Novemba 25, 2026) wakati akisikiliza kero za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ifakara, Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, ambapo aliwaagiza viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara watekeleze hukumu ya mahakama kuhusu nyumba ya mwananchi iliyobomolewa mwaka 2017.

“Haya mambo yanatengeneza chuki isiyo na sababu. Kama mnadhani mahakama ya mwanzo ama mahakama ya wilaya haijahukumu vizuri, hata kama wewe ni Serikali, unatakiwa ukate rufaa.”

Dkt. Mwigulu alitoa kauli hiyo baada ya mwananchi Yusuf Faya kulalamika kuwa halmashauri hiyo haikutekeleza hukumu iliyotolewa kufuatia kubomolewa kwa nyumba yake.

Baada ya mwanasheria wa halmashauri kusoma hukumu hiyo, ilibainika kuwa ubomoaji ulifanyika kinyume cha sheria na halmashauri iliagizwa kufanya tathmini ya nyumba iliyobomolewa, kulipa fidia na gharama za kesi pamoja na kuacha kumbughudhi mwananchi huyo.

Waziri Mkuu alihoji sababu za halmashauri kutotekeleza hukumu hiyo licha ya kutokata rufaa na kusisitiza kuwa hakuna kiongozi mwenye mamlaka ya kubatilisha hukumu ya mahakama kwa utashi wake. “Haya, nendeni mkatekeleze hukumu ya mahakama hiyo,” alisema.

Akijibu agizo hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Pili Kitwana, alikiri kuwepo kwa makosa ya kutotekeleza hukumu hiyo na kuahidi kuwa halmashauri itaitekeleza kama mahakama ilivyoamua.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu aliagiza kusitishwa kwa hatua za kubomoa nyumba ya Bibi Pili Mavimba, ambaye alilalamika kuwa alikuwa akitishiwa kuondolewa katika nyumba aliyokuwa akiishi hapo Ifakara mjini tangu mwaka 1958 kutokana na mgogoro wa umiliki uliotokana na masuala ya mirathi.

Baada ya kupitia nyaraka na kusikiliza maelezo ya viongozi, Waziri Mkuu aliagiza masuala ya kisheria yanayohusu umiliki wa eneo hilo yashughulikiwe ili bibi huyo apatiwe hati ya umiliki na kuondokana na usumbufu, kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2024.

Pia, alimwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, ashirikiane na Katibu Tawala na wataalamu wa ardhi kupima maeneo yanayogombaniwa na familia ya marehemu Omari Mtenga ili mgawanyo wa shamba la ekari tano utekelezwe kwa mujibu wa hukumu ya mahakama.

“Haya, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, hebu tusaidie kusimamia Katibu Tawala na mtu wa ardhi waende na vipimo, wawapimie kufuatana na maelekezo ya mahakama, ili tumalize huo mzizi wa fitina,” alisema.

Dkt. Mwigulu alisisitiza kuwa mhimili wa mahakama unapaswa kuheshimiwa na kwamba Serikali na watendaji wake wana wajibu wa kutekeleza hukumu zilizotolewa au kutumia taratibu za kisheria za kukata rufaa pale wanapokuwa hawajaridhika nazo.