▪ Aitaka TAKUKURU ifuatilie migogoro ya wakulima na wafugaji

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemwelekeza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, asimamie mapitio ya ushuru wa mazao katika halmashauri za mkoa huo ili kuhakikisha viwango vinavyotozwa vinazingatia uwezo wa wananchi na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mkuu alitoa maelekezo hayo jana (Jumatano, Novemba 25, 2026) katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa CCM, Tangani, Ifakara Mji, mkoani Morogoro, wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Kilombero, Abubakari Damian Asenga, kuhusu kukithiri kwa ushuru kwenye mazao.

“Nimemwachia Mkuu wa Mkoa, atapita halmashauri zote hizi ili kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhusu ushuru.”

Dkt. Mwigulu alisema Serikali inatambua umuhimu wa halmashauri kukusanya mapato kwa ajili ya kutoa huduma, lakini ukusanyaji huo lazima uzingatie mazingira halisi ya wananchi bila kuwaumiza wakulima wadogo. “Lazima muangalie hawa watu waende kwa makundi. Mwenye nusu gunia, mwenye ndoo tatu, mwenye gunia, mwenye magunia 50 au mwenye magunia 100.”

Alisema si sahihi mkulima mwenye gunia moja kubebeshwa mzigo wa ushuru kwa uwiano sawa na mfanyabiashara mwenye magunia 100. Alionya kuwa vikwazo vingi vya biashara vinaweza kuwafanya wanunuzi kukwepa maeneo husika na hivyo kupunguza mapato ya halmashauri.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimtaka Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa wa Morogoro afuatilie kesi zinazohusiana na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, na akaonya dhidi ya mauaji, rushwa na vitendo vya uvunjifu wa sheria vinavyoweza kuchochea visasi.

“Sasa Kamanda wa TAKUKURU, fuatilia kesi zote hizi za mambo yanayohusu migogoro ya ardhi, wakulima, wafugaji, hebu zifuatilieni zote. Lazima haki za wanyonge zilindwe.”

Alisisitiza kuwa migogoro hiyo inapaswa kutatuliwa kwa kufuata sheria na kwamba hakuna mwananchi anayepaswa kutumia uwezo wake wa kifedha kuwakandamiza wengine.