NA FAUZIA MUSSA

Viongozi wa vikundi vya wanawake wametakiwa kusimamia matumizi sahihi ya fedha za mikopo wanazopatiwa kwa kuzielekeza katika shughuli za uzalishaji mali na miradi ya maendeleo badala ya kuzitumia katika matumizi yasiyo na tija ikiwemo kufanya harusi na kuandaa chai.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Siti Abasi Ali, wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa wakufunzi wa maafisa waalimu wa vikundi vya wanawake, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Tumekuja, Wilaya ya Mjini, Unguja.

Amesema baadhi ya wanawake wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutofikia malengo yaliyokusudiwa kupitia mikopo wanayoipata kutokana na kutokuwa na usimamizi mzuri wa fedha hizo, hali inayoweza kudhoofisha juhudi za kuwawezesha kiuchumi.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wakufunzi hao kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa viongozi wa vikundi kuhusu matumizi bora ya mikopo, usimamizi wa fedha na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi ili wanawake waweze kunufaika na fursa hizo na kujikwamua kiuchumi.

Aidha, ameipongeza Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika utekelezaji wa Mradi wa PAMOJA, akieleza kuwa ushirikiano huo una mchango mkubwa katika kuwawezesha wanawake kujiajiri, kuanzisha miradi ya biashara na kukuza uchumi kupitia vikundi vyao.

Kwa upande wake, Ali Wadi Makame kutoka Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania (PAMOJA), amesema mradi huo unalenga kuimarisha uwezo wa vikundi vya wanawake katika matumizi na usimamizi wa fedha pamoja na kuongeza ufanisi katika shughuli zao za uzalishaji mali.

Amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo maafisa waalimu walioteuliwa ili waweze kutoa elimu na mwongozo kwa viongozi wa vikundi vya wanawake kuhusu namna bora ya kuendesha na kusimamia vikundi vyao, hatua itakayosaidia kuongeza tija na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Naye mmoja wa wakufunzi wa vikundi vya wanawake Zanzibar, kwa niaba ya wenzake, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa kwa kuhakikisha wanawaelimisha na kuwasaidia viongozi wa vikundi kusimamia vizuri fedha za mikopo wanazopatiwa ili ziweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Mafunzo hayo ya siku tano yameandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mradi wa PAMOJA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, yakishirikisha maafisa waalimu wa vikundi vya wanawake kutoka Unguja na Pemba.