Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akizungumza wakati akifungua Mkutano wa 39 wa Mwaka wa Wahasibu katika Hoteli ya APC, Bunju, jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) 

Na. Josephine Majura na Asia Singano, WF – Dar Es Salaam

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deagratius Luswetula (Mb), ameitaka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), kuendelea kuimarisha hatua za kinidhamu dhidi ya wahasibu na wakaguzi wanaokiuka maadili ya taaluma hiyo ili kudhibiti upotevu wa mapato na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Mhe. Luswetula (Mb), alitoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa 39 wa Mwaka wa Wahasibu katika Hoteli ya APC, Bunju, jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).

Alisema NBAA inapaswa kuchunguza kwa kina tuhuma za ukiukwaji wa maadili na kuchukua hatua zinazolingana na uzito wa makosa yaliyothibitishwa, kwa kuzingatia haki na ushahidi.

Aliwataka wataalamu wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na kufuata sheria na taratibu za taaluma yao ili kuendelea kulinda mali za umma.

‘’Nawahimiza wahasibu kukataa shinikizo la kuficha madeni, kubadilisha tarehe za nyaraka au kuthibitisha kazi ambazo hazijafanyiwa uhakiki, saini ya mkaguzi kwenye taarifa za fedha inapaswa kuungwa mkono na ushahidi wa kutosha’’ alisema Mhe. Luswetula.

Pia aliwataka waajiri na viongozi wa kampuni za ukaguzi kuwapa watumishi wao muda na mazingira bora ya kutekeleza majukumu yao kwa usahihi, kusikiliza hoja zao na kuhakikisha changamoto za kitaaluma zinapatiwa majibu yanayotegemea ushahidi.

Katika hatua nyingine, aliipongeza NBAA kwa kuanzisha mfumo wa NBAA Verification Number (NBAAVN), unaowezesha uhakiki wa taarifa za fedha zilizokaguliwa. Alihimiza kampuni za ukaguzi kuwasilisha taarifa hizo kwa wakati na kuzitaka benki, taasisi za fedha na mamlaka za umma kutumia mfumo huo kuthibitisha uhalali wa taarifa hizo kabla ya kufanya maamuzi.

Kuhusu matumizi ya teknolojia, alisema uchanganuzi wa takwimu, mifumo ya kidijitali na akili unde vinaweza kuboresha ukaguzi na kubaini miamala isiyo ya kawaida, lakini wahasibu na wakaguzi wanapaswa kuendelea kuwajibika katika kuhakiki ushahidi, kulinda taarifa za siri na kutumia uamuzi wa kitaaluma.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na NBAA kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, ubora wa taarifa za kifedha na maendeleo ya kitaaluma ili kuunga mkono utekelezaji wa Dira 2050.

Alisisitiza kuwa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, ni muhimu kutathmini si kiasi cha fedha kilichotumika pekee, bali pia kama mradi umekamilika, mali iliyojengwa inaweza kutunzwa na wananchi wanapata huduma zilizokusudiwa.

Aidha, aliipongeza NBAA kwa kuendesha CPA Sustainability Day Novemba 24, 2026, katika Hospitali ya CCBRT na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala, akisema hatua hiyo inaonesha mchango wa taaluma hiyo katika ustawi wa jamii.

Awali akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Mzenzi, alisema imani ya umma ndiyo msingi wa taaluma ya uhasibu na ukaguzi na inajengwa kupitia ubora wa kazi za wahasibu na wakaguzi. 

Kuhusu usimamizi wa fedha za umma Prof. Mzenzi alisema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hauwezi kufanikiwa bila usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma.

‘’Natoa wito kwa maafisa masuuli na wahasibu wa sekta za umma na binafsi kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani, kuandaa taarifa sahihi za fedha kwa wakati na kuchukua hatua zinazostahili kutekeleza mapendekezo ya wakaguzi’’ alisema Prof. Mzenzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Utawala ya NBAA, CPA Prof. Sylvia Shayo Temu, alitoa wito kwa wahasibu na wakaguzi wa hesabu nchini kubadili namna wanavyotekeleza majukumu yao kwa kutumia maarifa, teknolojia na ubunifu kuleta matokeo yanayopimika katika maendeleo ya uchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

‘’Taaluma ya uhasibu inapaswa kwenda zaidi ya kuandaa taarifa za fedha na badala yake kuwa mshirika muhimu katika mageuzi ya uchumi, kuimarisha utawala bora na kuongeza uwajibikaji katika taasisi’’ alisema Prof. Temu.

Mkutano huo wa siku tatu, unaofanyika Novemba 25 hadi 27, 2026, umebeba kaulimbiu “From Insights to Impacts: Driving Innovation and Sustainability in the Accountancy Profession for Dira 2050” na unajadili ubunifu, teknolojia, uendelevu, ubora wa ukaguzi na usimamizi wa fedha za umma.

Mkutano huo umewakutanisha wahasibu, wakaguzi wa hesabu, wawakilishi wa taasisi za Serikali, sekta binafsi, kampuni za ukaguzi na taasisi za kitaaluma kutoka Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akipokea Tuzo ya kutambua mchango wake wa ushiriki katika mkutano huo wa 39 wa Mwaka wa Wahasibu, alipofungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), CPA Prof. Sylvia Shayo Temu, wakati akipokelewa katika Hoteli ya APC, Bunju, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kufungua Mkutano wa 39 wa Mwaka wa Wahasibu, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), na Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), CPA Prof. Sylvia Shayo Temu wakimtunuku tuzo ya kuthamini mchango wake katika waaluma ya Wahasibu na Wakaguzi nchini aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Pius Maneno wakati wa Mkutano wa 39 wa Mwaka wa Wahasibu, unaofanyika katika Hoteli ya APC, Bunju, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), CPA Prof. Sylvia Shayo Temu, akizungumza wakati wa kumkaribisha, Mgeni rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), kufungua Mkutano wa 39 wa Mwaka wa Wahasibu.

Washiriki wa Mkutano wa 39 wa Mwaka wa Wahasibu, wakifuatilia mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya APC, Bunju, jijini Dar es Salaam, uliowakutanisha wahasibu, wakaguzi wa hesabu, wawakilishi wa taasisi za Serikali, sekta binafsi, kampuni za ukaguzi na taasisi za kitaaluma kutoka Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) Katikati walioketi, akiwa katika picha ya pamoja na sekretarieti ya maandalizi ya Mkutano wa 39 wa Mwaka wa Wahasibu (waliosimama), baada ya kufungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).

(Picha na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, WF Dar Es Salaam)