Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amemuondoa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Manyara, Mhandisi Dutu Masele, na kuelekeza kuteuliwa kwa Meneja mwingine kuchukua nafasi yake ili kuboresha usimamizi na kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya barabara mkoani humo.
Aidha, Waziri Kadogosa ameelekeza kuondolewa kwa Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo cha TANROADS mkoani humo kutokana na kushindwa kusimamia kwa karibu mkandarasi anayetekeleza kazi za ukarabati na matengenezo ya barabara ya Gehandu–Babati.
Maelekezo hayo yametolewa wakati Waziri Kadogosa alipokuwa akikagua maendeleo ya ukarabati na matengenezo ya barabara hiyo inayotarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2027, ambapo alieleza kutoridhishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa kazi licha ya fedha za mradi kuanza kupatikana tangu mwezi Agosti mwaka huu.
Amesema si jambo la kuridhisha kuona barabara hiyo, ambayo ina umuhimu mkubwa kiuchumi na inayounganisha kanda tatu, ikiwa katika hali isiyoridhisha wakati Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha miundombinu ya barabara nchini.
“Lazima nikiri ukweli kwamba kazi inayoonekana hapa haiendani na kasi iliyotakiwa. Kwa sababu hiyo, nimemrudisha Meneja wa TANROADS makao makuu na tutaleta mwingine. Serikali inatarajia kuona mabadiliko makubwa katika utekelezaji wa mradi huu,” amesisitiza Kadogosa.
Vilevile, amemuagiza Mkurugenzi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi pamoja na Mkurugenzi wa Matengenezo kutoka TANROADS kufika mara moja mkoani Manyara ili kuongeza nguvu katika usimamizi wa kazi hizo na kuweka mikakati madhubuti ya kuharakisha ukarabati na matengenezo ya barabara hiyo.
Ameelekeza pia kuwekwa kwa timu za wakandarasi katika maeneo yenye changamoto kubwa ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa kasi inayotakiwa na kukamilika kwa wakati, huku usimamizi na uwajibikaji vikiimarishwa.
Waziri Kadogosa amesisitiza kuwa barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kiuchumi kutokana na kupitisha takribani magari elfu nne na zaidi, hivyo kuchelewa kukamilisha matengenezo yake kunaathiri shughuli za usafirishaji na uchumi wa Mikoa mingi.

