Amtaka Naibu Waziri wa Ujenzi apige simu ‘live’ na kutoa majibu

WAZIRI MKUU Dkt Mwigulu Nchemba amesema haridhishwi na sababu zinazotolewa na viongozi kuhusu ucheleweshaji wa kivuko cha Kikove hadi Mlimba na akataka apewe majibu ya papohapo ni lini kivuko hicho kitafikishwa wilayani humo ili kianze kutoa huduma kwa wananchi.

Akizungumza na wananchi wa Malinyi leo (Jumanne, Novemba 24, 2026) katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Toboatobo, wilayani Malinyi, mkoani Morogoro Dkt. Mwigulu amesema haikubaliki wananchi kuendelea kupata shida ya usafiri wakati fedha za Serikali zimeshalipwa kwa ajili ya kivuko hicho.

Waziri Mkuu amesema mradi wa kivuko cha Kikove umedumu kwa karibu miaka tisa, na akataka majibu ya uhakika kuhusu lini kivuko hicho kitafikishwa Mlimba. “Mheshimiwa Naibu Waziri sijaridhika na maelezo yako kuhusu hiki kivuko. Hebu mpigie simu mtendaji wa TEMESA na umuweke kwenye kipazasauti ili wananchi wasikie ni lini hasa kivuko hiki kitafika hapa Malinyi.”

“Mmesema kivuko kimekamilika. Na sasa kama kimekamilika kinafanya nini huko? Nataka kujua kinakuja lini. Mimi sitaki ngonjera ngonjera. Miaka tisa hatuwezi tukaelezea jambo kwa wiki moja tena. Fedha ilishalipwa. Kivuko kimekaa muda mrefu. Wananchi hawa wanapata shida,” amesema.

Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Malinyi, Dkt. Mecktridis Mdaku, aliyesema mradi huo ulioanza mwaka 2017 na ukatarajiwa kukamilika mwaka 2020, umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara, hali inayowalazimu wananchi wanaosafiri kati ya Malinyi na Mlimba kutumia njia ndefu kupitia Ifakara.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema kivuko kimekamilika na maegesho ya upande wa Malinyi yako tayari, huku fedha zikiwa zimetolewa kwa ajili ya kazi zilizobaki kukamilisha maegesho ya upande wa Mlimba.

Katika mazungumzo hayo, Mtendaji huyo alisema kazi zilizobaki zinatarajiwa kukamilika Desemba 30, mwaka huu, na kivuko kitafikishwa Mlimba Januari 5, 2027, kwa ajili ya maandalizi ya kuanza kutoa huduma.

Waziri Mkuu pia amewaonya wakandarasi wanaopokea fedha za Serikali lakini wakashindwa kutekeleza miradi kwa wakati, akisisitiza kuwa fedha za umma lazima zitumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa.

Kuhusu migogoro ya mipaka ya hifadhi, Dkt. Mwigulu amesema Serikali itapokea taarifa ya timu ya mawaziri nane Novemba 29, 2026, kabla ya viongozi wa sekta husika kwenda katika maeneo yenye migogoro kusikiliza malalamiko ya wananchi na kupitia mipaka inayolalamikiwa.

Amesema wananchi watapata nafasi ya kueleza changamoto wanazokabiliwa nazo na kuonyesha maeneo ambayo wanadai mipaka imebadilishwa, ili Serikali ifanye tathmini na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria