Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), amezitaja fursa za kibiashara zilizopo nchini Tanzania katika Jukwaa la Maendeleo ya Biashara Afrika (ATDF 2026), akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya viwango na uzingatiaji wa masharti ya Afya ya Mimea na Wanyama (SPS) ili kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa barani Afrika katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Mhe. Londo aliyasema hayo leo wakati akishiriki kikao cha 14 cha Jukwaa la Maendeleo ya Biashara Afrika, kilichofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, chenye mada isemayo Mtego wa Viwango (The Standards Trap), ambapo alieleza hatua zinazopaswa kuchukuliwa na nchi za Afrika kuondoa vikwazo vinavyozuia ukuaji wa biashara na upanuzi wa masoko.

Amesema nchi za Afrika zinapaswa kuoanisha viwango vya kitaifa na vile vya kikanda na kimataifa ili kupunguza vikwazo vya kiufundi vinavyozuia biashara na kurahisisha bidhaa zinazozalishwa barani humo kuingia katika masoko mbalimbali.

Alibainisha kuwa kuimarisha miundombinu ya ubora, ikiwemo huduma za upimaji, uthibitishaji, ukaguzi na uidhinishaji wa uwezo wa taasisi za upimaji, ni hatua muhimu katika kuhakikisha bidhaa za viwandani na mazao yanayozalishwa Afrika zinakidhi matakwa ya masoko.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuzijengea uwezo biashara ndogo na za kati (MSMEs) katika masuala ya viwango, ubora, vifungashio na uthibitishaji wa bidhaa ili ziweze kushiriki kikamilifu katika minyororo ya thamani na kunufaika na fursa za biashara zilizopo.

Akizungumzia fursa za kukuza biashara ya kikanda, Mhe. Londo amesema makubaliano ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yanatoa fursa muhimu kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania kupanua masoko, kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Amesema matumizi sahihi ya fursa hizo yanahitaji ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, pamoja na uwekezaji katika uzalishaji wenye tija na uongezaji thamani wa bidhaa ili kuongeza uwezo wa Tanzania kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na ugavi, pamoja na kuwezesha wafanyabiashara kupata huduma za viwango na uthibitishaji kupitia taasisi husika zikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Amesema hatua hizo zinalenga kuongeza uwezo wa viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa bora, kuongeza thamani ya rasilimali za nchi na kupanua mauzo ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya Afrika na kimataifa.

Jukwaa hilo linawakutanisha Mawaziri wa Viwanda, Biashara na Mtangamano wa Kibiashara kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa lengo la kujadili fursa za biashara barani humo na kuweka mikakati ya kukabiliana na vikwazo vinavyoathiri biashara, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kupanua masoko ya bidhaa za Afrika.