Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, Bi. Emma Mwasyoge, akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji katika  kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026
………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM 
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefanikisha kuimarisha ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, ambapo jumla ya Shilingi bilioni 1.17 zimekusanywa katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Bi. Emma Mwasyoge, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya taasisi hiyo na uongozi wa manispaa katika kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali.
Mwasyoge amesema fedha hizo zimepatikana kupitia ufuatiliaji wa ulipaji wa Ushuru wa Huduma (Service Levy) pamoja na usimamizi wa utozaji wa faini kwa wafanyabiashara wanaokiuka taratibu zilizowekwa.
Mwasyoge ameeleza kuwa katika zoezi la uhakiki wa taarifa za walipa kodi, jumla ya makampuni 94 yalifikiwa kwa ajili ya kukagua malipo ya ushuru wa huduma kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, ambapo 50 yalibainika kuwa na madeni.
Amesema baada ya kufuatiliwa na kuchukuliwa hatua stahiki, makampuni hayo yalilipa jumla ya Shilingi bilioni 1.066, fedha ambazo zimeongeza uwezo wa manispaa kupata mapato yake halali na kupunguza mianya ya upotevu wa rasilimali za umma.
Aidha, amesema TAKUKURU kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke pamoja na manispaa hiyo, ilisimamia ukusanyaji wa faini kwa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao katika maeneo yasiyoruhusiwa, yakiwemo Tandika, Mbagala, Kongowe na Buza, hatua iliyowezesha kukusanya Shilingi milioni 104.6.
Mwasyoge amesema taasisi hiyo imefanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika miradi mitano ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 13.24, iliyotekelezwa katika Manispaa za Temeke na Kigamboni.
Amefafanua kuwa miradi mitatu yenye thamani ya Shilingi bilioni 12.239 ilikuwa katika Manispaa ya Temeke, huku miwili yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.001 ikitekelezwa Kigamboni.
“Ukaguzi huo ulibaini changamoto mbalimbali, zikiwemo kuchelewa kuanza na kukamilika kwa baadhi ya miradi, ucheleweshaji wa vifaa vya ujenzi kufikishwa katika maeneo ya kazi pamoja na baadhi ya wakandarasi kutokuwa na usajili kutoka mamlaka husika, ikiwemo OSHA na Bodi ya Wakandarasi” 
Amesema TAKUKURU iliendesha semina mbili kwa madiwani wa Temeke na Kigamboni kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu Programu ya TAKUKURU Rafiki, ambapo katika kipindi hicho vikao 12 vya programu hiyo vilifanyika na kuwezesha kubaini kero mbalimbali za wananchi.
Ameongeza kuwa katika kuimarisha elimu ya mapambano dhidi ya rushwa, taasisi hiyo imeendesha semina 47, mikutano ya hadhara 32, kuanzisha na kuimarisha Klabu za Wapinga Rushwa 84 pamoja na kushiriki maonesho sita.
Pia, amesema wanafunzi 226 wa vyuo vya elimu ya juu wamepatiwa elimu ya maadili na madhara ya rushwa, huku vyuo vitatu vya DUCE, TIA na LITA, Kampasi ya Temeke, vikikabidhiwa mipira na jezi ili kutumia michezo kuhamasisha ushiriki wa vijana katika mapambano hayo.
Akizungumzia mikakati ya robo ya Oktoba hadi Desemba 2026, Mwasyoge amesema TAKUKURU itaendelea kutoa elimu kwa umma, kufanya uchambuzi wa mifumo katika maeneo yenye viashiria vya rushwa, kufuatilia miradi ya maendeleo na kushughulikia malalamiko yanayopokelewa kwa mujibu wa sheria.
Amesema taasisi hiyo pia itafuatilia maandalizi ya kukabiliana na mvua kubwa na athari za El Niño kwa kushirikiana na Manispaa ya Temeke pamoja na wadau wengine, hususan katika maeneo hatarishi kwa mafuriko, ili kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya kukabiliana na majanga zinatumika kwa uwazi na malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kuzuia rushwa kwa kutoa taarifa kupitia simu ya bure namba 113 au kufika katika ofisi za TAKUKURU zilizo karibu nao, akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mmoja.