Benki ya NMB inaendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika kukuza vipaji na bunifu za vijana, kwa kuwaunganisha na fursa za ushauri wa kitaalamu, ukuzaji wa biashara na upatikanaji wa soko kupitia teknolojia.
Akizungumza katika maonesho ya bunifu za wanafunzi ya NMB–UDSM Innovation Showcase, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Rasilimali Watu na Vitengo vya Biashara wa NMB, Erica Hanson, amesema kupitia NMB Innovation Hub na ushirikiano na idara mbalimbali za biashara za benki hiyo, wabunifu watapata fursa ya kuboresha bunifu zao na kuendeleza bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji ya soko.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa UDSM anayeshughulikia Utafiti na Ubunifu, Dkt. Cosmas Mushi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya vyuo vikuu na sekta binafsi katika kuongeza wataalamu wa teknolojia nchini, akieleza kuwa bunifu zilizowasilishwa zimeendelezwa kwa takribani miezi mitatu kutoka hatua ya mawazo hadi kuwa bidhaa zinazoweza kutathminiwa.
Maonesho hayo, yaliyohudhuriwa pia na Kaimu Mkuu wa Idara ya Ubunifu wa NMB, Innocent Shirima, yanaakisi dhamira ya taasisi hizo katika kuwawezesha vijana kutumia maarifa ya darasani kujenga biashara, kutengeneza fursa za ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

