Na: Mwandishi Maalum
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Omari Sukari amewahimiza wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kupima afya ya moyo katika kambi maalumu ya uchunguzi wa afya inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita (GRRH) ili kutambua changamoto za kiafya mapema na kupata matibabu kwa wakati.
Kambi hiyo maalumu inafanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea hafla ya chakula cha jioni kuchangisha fedha kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.
Akizungumza wakati wa kufungua kambi hiyo Dkt. Sukari aliipongeza JKCI kwa kujitoa na kusogeza huduma za bingwa bebezi za magonjwa ya moyo karibu na wananchi.
“Tunawashukuru sana JKCI kwa kuleta huduma hii Mkoani Geita, ni muhimu wananchi watambue kuwa magonjwa ya moyo yanahitaji uchunguzi wa mapema na tunapowaletea wataalamu karibu na maeneo yao tunawapa nafasi ya kujua hali zao za afya na kupata msaada kwa wakati”, alisema Dkt. Sukari.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Winnie Masakuya alisema kambi hiyo ina umuhimu mkubwa kwa watoto wenye magonjwa ya moyo kwa kuwa inatoa fursa ya kuwafikia na kuwafanyia uchunguzi ili kubaini changamoto zao na kuwapatia matibabu mapema.
“Afya ya moyo wa mtoto ni muhimu katika ukuaji na maisha yake, tunawahimiza wazazi na walezi wasisubiri mpaka changamoto ya mtoto iwe kubwa watumie fursa kuja kwenye kambi hii ili watoto wao wafanyiwe uchunguzi na wataalamu waweze kutathmini hali zao na kushauri hatua zinazofaa”, alisema Dkt. Masakuya.
Kupitia kambi hiyo wananchi wa mkoa wa Geita watapata fursa ya kupata huduma za uchunguzi wa afya ya moyo ikiwome kufanyiwa vipimo vya moyo, shinikizo la damu na sukari kwenye damu.

