NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, ameunga mkono juhudi za wananchi wa Kijiji cha Sadani, Kata ya Masaka, kwa kutoa mifuko 50 ya saruji itakayosaidia kuharakisha ujenzi wa ofisi ya kijiji hicho.
Msaada huo unalenga kuimarisha hatua za ujenzi wa jengo hilo ambalo linatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya shughuli za kiutawala na utoaji wa huduma kwa wananchi, huku ukiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyokuwa ameitoa kwa wakazi wa kijiji hicho.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Sadani, Devis Msela, amesema mchango huo umeongeza nguvu katika mradi wa ujenzi ambao ulianza mwaka huu, akimpongeza mbunge kwa kutimiza alichowaahidi wananchi.
Msela amesema kukamilika kwa ofisi hiyo kutasaidia kuondoa changamoto ya mazingira duni ya kiutendaji iliyokuwa ikiwakabili viongozi wa kijiji, wakiwemo mwenyekiti, mtendaji na wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji, kutokana na ofisi ya awali kutokuwa katika hali inayokidhi mahitaji yao.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Masaka amempongeza Kiswaga kwa kuendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo katika kata hiyo, akimtaja kuwa kiongozi anayejidhihirisha kwa vitendo kupitia ushiriki wake katika kutatua changamoto za wananchi.
Wananchi wa Sadani wameeleza matumaini yao kuwa ujenzi wa ofisi hiyo utakapokamilika, utakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya kazi kwa viongozi wa kijiji, kuongeza ufanisi wa shughuli za kiutawala na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

