Na Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto katika Wizara ya Afya, Dkt. Ahmad Makuwani, amezipongeza taasisi za Serikali zikiwemo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wizara ya Maji na Wizara ya Ujenzi kwa mchango wake katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kupitia usambazaji wa umeme, maji safi na ujenzi wa miundombinu bora ya barabara nchini.
Dkt. Makuwani amesema upatikanaji wa huduma hizo za msingi umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utoaji wa huduma za afya, hususan katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, kwa kuwa umeme unawezesha huduma za upasuaji na matibabu ya dharura, maji yanasaidia usafi na kuzuia maambukizi, huku barabara zikirahisisha usafirishaji wa wagonjwa na huduma za rufaa.
Akizungumza wakati wa kufungua semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), jijini Dar es Salaam, Novemba 23, 2026, Dkt. Makuwani alisema mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya nchini.
Alisema hadi mwaka 2024/2025 vijiji vyote 12,318 nchini, sawa na asilimia 100, vilikuwa vimeunganishwa na nishati ya umeme, huku vijiji 10,779 kati ya hivyo vikiwa vimefikiwa na huduma ya maji safi, sawa na asilimia 83. Aidha, alisema mtandao wa barabara zinazopitika wakati wote wenye urefu wa kilometa 144,300 umechangia kurahisisha safari za rufaa na kuwawezesha wagonjwa kupata huduma kwa wakati.
Dkt. Makuwani alisema mafanikio hayo yanaenda sambamba na juhudi za Serikali katika kutekeleza mikataba miwili ya uwajibikaji iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama aliyoizindua mwaka 2018 akiwa Makamu wa Rais na mkataba wa kuimarisha lishe ulioingiwa mwaka 2022.
Alisema mikataba hiyo imekuwa chachu ya uwajibikaji kwa viongozi wa mikoa katika kusimamia huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto pamoja na lishe, na kuchangia kuimarika kwa upatikanaji wa dawa, miundombinu na huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini.
Alibainisha kuwa bajeti ya sekta ya afya imeongezeka kutoka Shilingi trilioni 2.46 mwaka 2023/2024 hadi Shilingi trilioni 3.7 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, huku upatikanaji wa dawa za afya ya uzazi, mama na mtoto ukifikia zaidi ya asilimia 85 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Alisema pia Serikali imeongeza vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo zahanati zimeongezeka kutoka 4,127 hadi 6,589, vituo vya afya kutoka 535 hadi 1,067 na hospitali za wilaya kutoka 77 hadi 194 kati ya mwaka 2015/2016 na 2024/2025, hatua iliyowezesha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania kupata huduma za afya ndani ya umbali wa kilometa tano.
Aidha, alisema magari ya kubebea wagonjwa yameongezeka kutoka 540 mwaka 2021 hadi 1,113 mwaka 2026, huku wodi maalumu za watoto wachanga zikiongezeka kutoka 14 mwaka 2018 hadi 438 mwaka 2025, hatua iliyoongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma kwa watoto wanaozaliwa wakiwa na changamoto mbalimbali za kiafya.
Aliongeza kuwa mfumo wa rufaa wa kielektroniki wa m-Mama ulioanzishwa mwaka 2020 umewezesha kusafirisha wagonjwa 250,000 hadi Agosti 2026, ambapo asilimia 81 ni akina mama, asilimia 18 watoto wachanga na asilimia moja ni mama na mtoto mchanga kwa pamoja.
Akizungumzia mwenendo wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, Dkt. Makuwani alisema kiwango cha wajawazito wanaohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza kimefikia asilimia 86 kutoka asilimia 84 mwaka 2022, huku wanaohudhuria kliniki angalau mara nne wakiongezeka kutoka asilimia 65 hadi asilimia 81.
Alisema kiwango cha wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya kimeongezeka kutoka asilimia 81 mwaka 2022 hadi asilimia 85, huku watoto 71,000 wakipata huduma katika wodi maalumu za watoto wachanga mwaka 2025 na wengine 91,000 wakihudumiwa katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2026.
Dkt. Makuwani alisema mafanikio hayo yamechangia kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi 104 mwaka 2022, huku vifo vya watoto vikishuka kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000 katika kipindi hicho.
Alisema kutokana na hatua hizo, Rais Samia ametambuliwa kimataifa kwa mchango wake katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, ikiwemo kutunukiwa tuzo ya Goalkeepers ya Gates Foundation Februari 2025 na kutambuliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika huduma za mama na mtoto.
Alisema Serikali sasa inaelekeza nguvu katika kufikia malengo ya mwaka 2030 ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hadi chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000, vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano hadi chini ya 25 kwa kila vizazi hai 1,000 na vifo vya watoto wachanga hadi chini ya 12 kwa kila vizazi hai 1,000.
Alifafanua kuwa mkutano wa tatu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto pamoja na Lishe, utakaofanyika Novemba 25 hadi 27, 2026, umeandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) pamoja na wadau wa maendeleo, ukiwa na lengo la kujadili mikakati ya kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuongeza uwajibikaji katika sekta hiyo. Rais Samia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, kufungua mkutano huo, kusaini mkataba wa pili wa uwajibikaji kwa wakuu wa mikoa na kuzindua ripoti ya hali ya vifo vitokanavyo na uzazi na watoto nchini.
Katika kuhitimisha, Dkt. Makuwani amevitaka vyombo vya habari kushiriki kikamilifu katika kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto, kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya ili kupata huduma bora bila kutumia gharama kubwa kutoka mifukoni mwao, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, wadau na jamii katika kuimarisha huduma hizo.

