Shirika la Posta Tanzania kupitia Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini limeendelea kuimarisha uwezo wake katika kusimamia na kupima utekelezaji wa majukumu yake kwa kutembelea wizara mbalimbali za Serikali kwa lengo la kujifunza mifumo ya kidijitali inayotumika katika ufuatiliaji na tathmini ya utendaji kazi.
Miongoni mwa Wizara zilizotembelewa ni Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Afya pamoja na Wizara inayosimamia masuala ya vijana.
Akizungumza kupitia Posta TV, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Shirika la Posta Tanzania, Bi. Zahra Kitara, amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa Shirika kutokana na fursa ya kujifunza namna taasisi hizo zinavyotumia mifumo ya kidijitali kukusanya taarifa, kufuatilia utekelezaji wa majukumu na kupima utendaji kazi.
Amesema maarifa yaliyopatikana kupitia ziara hiyo yatasaidia Shirika kuimarisha usimamizi wa utendaji kazi, kufuatilia utekelezaji wa mipango yake na kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa ufanisi.
Aidha, amesema matumizi ya mifumo hiyo yanatarajiwa kuwa na manufaa kwa wananchi kwa kuimarisha ufuatiliaji na ubora wa huduma mbalimbali za kiposta wanazopatiwa, kupitia usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa majukumu ya Shirika.

