Na Mwandishi wetu, Simiyu

WANANCHI wameendelea kuhamasishwa kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kutokana na athari zake kubwa kwa afya, ustawi wa familia na uchumi, sambamba na kutambua umuhimu wa Bima ya Afya kwa wote katika kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu.

Hayo yamesemwa na Dkt Juma Muna ambaye ni Mratibu wa magonjwa yasiyombukiza Mkoa wa Simiyu katika kipindi cha AFYA TALK cha Kituo Cha Redio Nyanza FM.

Dkt Muna amesema magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo shinikizo la juu la damu, kisukari, magonjwa ya moyo, saratani na magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji, yanaweza kusababisha madhara makubwa kiafya, hasa pale yanapochelewa kugunduliwa au mgonjwa anapokosa matibabu na ufuatiliaji wa mara kwa mara.

Amesema miongoni mwa athari kubwa za kiafya zinazoweza kusababishwa na magonjwa hayo ni kiharusi, mshtuko wa moyo, kushindwa kufanya kazi kwa figo, upotevu wa uwezo wa kuona, uharibifu wa mishipa ya fahamu, ulemavu wa kudumu na vifo vya mapema.

Dkt Muna ambaye pia ni mratibu huduma za Tiba Katika Hospital ya Rufaa Mkoa Simiyu alifafanua kuwa shinikizo la juu la damu lisilodhibitiwa linaweza kuharibu mishipa ya damu na kuongeza hatari ya kupata kiharusi, mshtuko wa moyo na magonjwa ya figo.

“Aidha, kisukari kisichodhibitiwa kinaweza kusababisha uharibifu wa macho, figo na mishipa ya fahamu, pamoja na vidonda vya miguu vinavyoweza kufikia hatua ya kukatwa kwa kiungo,” amesema.

Ameeleza kuwa baadhi ya magonjwa hayo huendelea bila kuonesha dalili za wazi katika hatua za awali, hali inayoweza kusababisha wananchi kutafuta matibabu baada ya kupata madhara makubwa. 

“Hivyo, uchunguzi wa afya wa mara kwa mara ni muhimu katika kutambua vihatarishi na magonjwa mapema ili Kila mwananchi kujua namba zake ikiwepo shinikizo la Damu, sukari katika damu, uzito na urefu, mafuta katika mzunguko wa damu ,mapigo ya moyo na mengine ili kuweza kugundua magonjwa haya yasiyombukiza mapema na kuzuia athari zake .

Amesema mbali na madhara ya kimwili, magonjwa yasiyoambukiza yanaweza kuathiri afya ya akili, kupunguza uwezo wa mtu kufanya kazi na kuongeza utegemezi ndani ya familia.

“Matibabu ya muda mrefu, matumizi ya dawa za kila siku na mahitaji ya huduma maalumu kama usafishaji damu kwa baadhi ya wagonjwa wenye figo zilizoshindwa kufanya kazi yanaweza kuongeza mzigo wa kifedha kwa familia,” amesema Dkt Muna.

Amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, Bima ya Afya kwa Wote ina umuhimu mkubwa katika kuimarisha ulinzi wa kifedha, kwa kupunguza hatari ya wananchi kulipia gharama kubwa za matibabu moja kwa moja kutoka mifukoni mwao, kulingana na huduma na masharti ya bima husika.

“Uwepo wa bima ya afya unaweza kusaidia wananchi kupata huduma za uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa magonjwa sugu, na hivyo kupunguza uwezekano wa kuchelewa kupata huduma kutokana na changamoto za kifedha,” amesema Dkt Muna.

Amesema wananchi wanashauriwa kuzingatia lishe bora, kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, kupunguza matumizi ya chumvi, kuepuka tumbaku, kuepuka matumizi hatarishi ya pombe na kufanya uchunguzi wa afya kwa wakati.