Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini leo, Novemba 22, 2026, kuelekea Addis Ababa, Ethiopia, kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Akiwa nchini humo, Rais Samia ambaye pia ni Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, atashiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026).
Katika mkutano huo, Rais Samia anatarajiwa kuzindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika, utakaotekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030.
Mpango huo unalenga kuongoza nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kufikia malengo yanayojulikana kama Sifuri Tatu (Three Zeros), ambayo ni kuhakikisha kila mwanamzito anajifungulia katika kituo cha kutolea huduma za afya akisaidiwa na mtaalamu, kukomesha vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika, pamoja na kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo.
Aidha, mpango huo unalenga kuongeza uwekezaji wa nchi wanachama na wadau wa maendeleo katika kupanua upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wanawake, watoto na vijana barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, uzinduzi wa mpango huo utafanyika Novemba 23, 2026.

