Mkutano wa Nane wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu Maji Chini ya Ardhi, umemalizika Novemba 20, 2026, jijini Dar es Salaam, kwa msisitizo wa kuimarisha usimamizi, matumizi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za maji chini ya ardhi.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Usimamizi wa Maji Chini ya Ardhi ya SADC (SADC-GMI), amewapongeza washiriki na kuwataka kuthamini na kulinda rasilimali za maji chini ya ardhi, akieleza kuwa ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha upatikanaji na usambazaji wa maji kwa jamii.
Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina ya nchi wanachama wa SADC kutunza na kuhifadhi matabaka ya miamba yanayohifadhi maji chini ya ardhi, ili kuhakikisha rasilimali hiyo inakuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Naye Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Robert Sunday, ameipongeza Taasisi ya SADC-GMI kwa maandalizi mazuri na mafanikio yaliyopatikana katika mkutano huo, uliowakutanisha wadau wa Sekta ya Maji kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.
Amewataka washiriki kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo maazimio na mapendekezo yote yaliyojadiliwa katika mkutano huo, na kusisitiza kuwa hatua hiyo itachochea matumizi bora, usimamizi madhubuti na uhifadhi endelevu wa rasilimali za maji chini ya ardhi katika nchi wanachama wa SADC.

