📍Mlandizi, Pwani

Serikali imeendelea na uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Maji nchini, ikiwemo wilaya ya Kibaha, ili kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama. 

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Kundo Andrea Mathew (Mb) akizungumza na wananchi wa Mlandizi wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Mwigulu Nchemba, amesema katika kipindi cha mwaka 2021–2025, Serikali imekamilisha miradi 11 ya maji yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 5.01, ambayo kwa sasa inatoa huduma kwa wananchi.

Ameeleza kuwa kutokana na uwekezaji huo, zaidi ya asilimia 87.5 ya wakazi wa Wilaya ya Kibaha wanapata huduma ya majisafi na salama. Aidha, amesema miradi mingine minane inaendelea kutekelezwa na inatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 2027..

Mhandisi Kundo amemshukuru Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi ya “kumtua mama ndoo ya maji kichwani” .

Kuhusu mradi wa maji kutoka Chalinze kuelekea vijiji vya Magindu na Lubunge, Waziri Kundo amesema mradi huo ulikamilika na kuanza kutoa huduma, lakini baadhi ya wafugaji waliingiza mifugo katika maeneo ya miundombinu ya maji na kusababisha uharibifu ambapo Wizara ya Maji inaendelea na majadiliano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kupata suluhisho la kudumu, ikiwemo kutenga maeneo maalumu kwa mifugo bila kuathiri miundombinu ya maji.

Vilevile, amesema Serikali inaendelea na usanifu wa mradi wa kusafirisha maji kutoka Mto Rufiji kwenda katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Lindi ambapo uwekezaji huo ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, Wilaya ya Kibaha na maeneo mengine nchini yanakuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji na kuondokana na changamoto ya upungufu wa huduma hiyo.