📍Chalinze
Serikali itahakikisha huduma ya majisafi na salama inawafikia wananchi wote wa mji wa Chalinze kwa asilimia 100 ambapo kwa sasa upatikanaji wa huduma hiyo ni asilimia 92.
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Andrea Mathew (Mb), akishiriki ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema hayo katika Wilaya ya Chalinze, Mkoa wa Pwani.
Amesema ongezeko la watu na uwekezaji wa viwanda katika eneo hilo limeongeza mahitaji ya maji, hivyo Serikali inaendelea kupanua mtandao wa usambazaji maji. Ameeleza kuwa miradi miwili ya maji inaendelea kutekelezwa, ukiwemo Mradi wa Maji wa Matipwili ambao utekelezaji umefika asilimia 82.
Amebainisha kuwa Serikali imetekeleza miradi 13 ya maji katika eneo la Chalinze yenye thamani ya shilingi bilioni 3.46, na miradi inayoendelea ikitarajiwa kukamilika ndani ya mwaka 2026-2027.
Amesisitiza kuwa Wizara ya Maji haitakuwa kikwazo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama.
Waziri Kundo amesisitiza umuhimu wa teknolojia kwa kufunga Dira za malipo kabla, kwani mfumo huo utasaidia kuboresha usimamizi wa matumizi ya maji, kuongeza ufanisi wa huduma na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa wananchi.

