Mwenyekiti wa WIMO, Mary James akizungumza kwenye maonesho hayo jijini Dar es Saalam

Afisa manunuzi wa kampuni hiyo, Anirudh Shekhawat akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam
………..
Na Happy Lazaro, Dar es Salaam.
TAASISI ya Wanawake waongezaji wa mnyororo wa dhamani ya madini Tanzania (WIMO) kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia uongezaji thamani wa madini ya vito yanayopatikana nchini, ikiwemo Tanzanite na Citrine, ambayo awali baadhi yake yalikuwa yakipuuzwa na kutupwa kutokana na kutotambuliwa kwa thamani yake.
Akizungumza kuhusu shughuli za Taasisi hiyo, Mwenyekiti wa WIMO, Mary James, amesema taasisi hiyo imekuwa ikijihusisha na uongezaji thamani wa madini ya vito kwa takribani miaka mitano hadi sita, hatua inayosaidia kuyabadilisha madini ya kawaida kuwa bidhaa zenye thamani kubwa zaidi sokoni.
Amesema wakati taasisi hiyo inaanza shughuli zake, kulikuwa na madini mengi ya vito ambayo hayakupewa kipaumbele na baadhi ya wachimbaji, lakini wanawake wa WIMO walitambua fursa iliyokuwapo na kuanza kuyachakata na kuyaongezea thamani ili yaweze kuvutia wanunuzi.
Akitolea mfano wa jiwe la Citrine, amesema madini hayo yanapopatikana katika hali yake ya kawaida yanaweza kuonekana kuwa na thamani ndogo, lakini kupitia ubunifu na uchakataji unaofanywa na wanachama wa WIMO, yanaweza kubadilika na kuwa bidhaa yenye mvuto na thamani kubwa zaidi.
Amesema ushiriki wao katika mikutano na maonesho ya sekta ya madini unawapa fursa ya kukutana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, kutangaza bidhaa zao na kupata masoko mapya, hasa ikizingatiwa kuwa soko la ndani la madini hayo bado ni dogo.
“mikutano hii inatusaidia pia kujenga mitandao ya kibiashara, kubadilishana mawasiliano na wadau wa kimataifa pamoja na kupata fursa za kuendeleza biashara zao kupitia uhusiano wanaouanzisha na washiriki kutoka mataifa mbalimbali.”amesema Mary .
Aidha Mary amewahimiza wanawake nchini kujitokeza na kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini, akisema bado wapo wanawake wengi ambao hawajatambua uwezekano wa kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali zinazohusiana na madini.
Amesema WIMO ni jukwaa la kuwaunganisha wanawake wenye nia ya kujifunza, kushirikiana na kujiendeleza katika sekta hiyo, huku akiwakaribisha wanawake kujiunga na chama hicho ili kwa pamoja waweze kuongeza thamani ya rasilimali za madini zinazopatikana nchini na kunufaika nazo kiuchumi
