Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo (Mb), amezindua ripoti ya utafiti kuhusu wafanyabiashara wadogo nchini, iliyolenga kufuatilia shughuli zao za kila siku ili kubaini hali halisi ya kifedha na mwenendo wa biashara zao.
Akizindua ripoti hiyo iliyoandaliwa na Taasisi ya FSDT jijini Dar es Salaam, Mhe. Londo amesema utafiti huo umechambua mwenendo wa biashara, usimamizi wa fedha na upatikanaji wa huduma mbalimbali za kibiashara, hivyo utasaidia kuzalisha takwimu zitakazoiwezesha Serikali na taasisi za fedha kuelewa mahitaji halisi ya wafanyabiashara wadogo, hususan wanawake na vijana.
Amesema ripoti hiyo imekuja wakati muafaka, kufuatia Serikali kuzindua Sera ya Maendeleo ya Ujasiriamali Ndogo na wa Kati, ambayo itasaidia kuweka mikakati madhubuti ya kuwaendeleza wajasiriamali hao kwa kutumia taarifa na matokeo ya tafiti kama hiyo.
Katika hafla hiyo, Mhe. Londo amesema utafiti huo utasaidia Serikali kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Ujasiriamali Ndogo na wa Kati pamoja na Mkakati wa Biashara, ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani wenye thamani ya Dola za Marekani trilioni moja.
Amesema utafiti umebaini kuwa asilimia 94 ya wafanyabiashara wana mapato yanayozidi gharama za biashara zao, ingawa mapato hayo hubadilika kutoka mwezi mmoja hadi mwingine. Aidha, asilimia 38 hutegemea akiba binafsi na asilimia 33 hukopa kwa ndugu na marafiki wanapokabiliwa na changamoto za kifedha.
Katika matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali, utafiti umebaini kuwa asilimia 72 ya miamala bado hufanyika kwa fedha taslimu, huku asilimia 40 ya wafanyabiashara wakitaja gharama kubwa za huduma hizo na asilimia 31 wakikabiliwa na changamoto ya ujuzi wa kuzitumia.
Aidha, Mhe. Londo amesema biashara zinazomilikiwa na wanaume katika utafiti huo hupata faida kwa wastani wa asilimia 73 zaidi ya zile zinazomilikiwa na wanawake.
Kutokana na matokeo hayo, amezitaka taasisi za fedha kubuni mikopo yenye masharti ya marejesho yanayozingatia mzunguko na hali halisi ya mapato ya wafanyabiashara wadogo, pamoja na kupanua upatikanaji wa mikopo ya muda mfupi, bima na huduma nyingine za kifedha.
Pia amezitaka taasisi za fedha na watoa huduma za teknolojia kuboresha mifumo ya malipo ya kidijitali ili iwe rahisi na nafuu kwa wafanyabiashara, huku mamlaka za udhibiti zikitakiwa kuweka mazingira rafiki kwa ubunifu wa huduma za kifedha na kuhakikisha ulinzi wa watumiaji.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha wanawake kupata mitaji, ujuzi wa usimamizi wa fedha na taarifa za masoko, huku akiwahimiza wafanyabiashara kutunza kumbukumbu sahihi na kusimamia vizuri fedha za biashara zao.
Awali, akizungumzia utafiti huo, Mtendaji Mkuu wa FSDT, Eric Masinda, amesema ulifanyika kwa kipindi cha miezi 14 chini ya uongozi wa Kamati ya Kitaalam iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Deogratias Macha.
Amesema utafiti huo ulifuatilia shughuli za kila siku za wafanyabiashara wadogo ili kuelewa hali zao halisi za kifedha na kibiashara, ikiwemo mapato na matumizi, usimamizi wa fedha, upatikanaji wa mikopo na huduma za kifedha, matumizi ya malipo ya kidijitali pamoja na changamoto wanazokutana nazo katika biashara zao.
Ameeleza kuwa vituo vitano vya biashara nchini vilitumika katika utafiti huo, ambavyo ni Mutukula mkoani Kagera, Kahama mkoani Shinyanga, Namanga mkoani Arusha, Tunduma mkoani Mbeya na Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Utafiti huo ulifanyika kwa kushirikiana na Trademark Africa (TMA), Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), huku ukipata ufadhili na uungwaji mkono wa Gates Foundation na Trademark Africa.
Wizara ya Viwanda na Biashara ilikuwa miongoni mwa wadau walioshiriki kutoa mchango wa kitaalamu na kusimamia utekelezaji wa utafiti huo kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, vyama vya wafanyabiashara na taasisi za kifedha.
Matokeo ya utafiti huo yanatarajiwa kusaidia Serikali na taasisi za kifedha kuboresha sera, kanuni na mifumo ya huduma za kifedha ili kukidhi mahitaji halisi ya wafanyabiashara wadogo na kuimarisha ukuaji wa biashara zao nchini.

