MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, ameahidi kushirikiana na Baraza la Madiwani pamoja na wataalamu wa Halmashauri hiyo kuhakikisha miundombinu ya elimu katika Shule ya Sekondari na Msingi Nyumbu inaboreshwa, ili kuimarisha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Ahadi hiyo ameitoa Novemba 20, 2026, wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miundombinu ya shule hizo zilizopo Kata ya Mkuza, ambapo amebainisha kuwa Shule ya Sekondari Nyumbu ina historia kubwa kitaaluma na inahitaji kuendelezwa ili kukidhi mahitaji ya elimu kwa ngazi ya juu zaidi.

Dkt. Mawazo amesema Manispaa ya Kibaha ina mpango wa kuelekeza fedha katika kuboresha miundombinu ya shule hiyo, ambayo inatarajiwa kupandishwa hadhi na kuwa na michepuo ya kidato cha tano na sita, hatua inayolenga kuongeza fursa za wanafunzi kupata elimu ya sekondari ya juu.

Katika hatua nyingine, wakati akikagua Shule ya Msingi Nyumbu, Meya huyo amebaini changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa jengo la utawala kwa walimu, na kuahidi kuichukulia changamoto hiyo kwa uzito na kushirikiana na wadau kuhakikisha inapatiwa ufumbuzi.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu pamoja na kuongeza idadi ya walimu, hivyo ni muhimu kwa Halmashauri na wadau kuendelea kushirikiana kutatua changamoto zilizobaki ili walimu wafanye kazi katika mazingira bora.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyumbu, Juma Mrope, shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kitaaluma, ikiwa na wastani wa ufaulu wa asilimia 94.2 katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2025.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyumbu, Hambali Mshana, amesema shule hiyo imepata wastani wa ufaulu wa asilimia 93 katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2026.