……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kuwa mfano katika uendelezaji wa miradi ya makazi bora na ya kisasa, hatua iliyovutia viongozi wa Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC) pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, Ardhi na TEHAMA ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, waliotembelea miradi ya Golden Premier Residence (GPR) na Kawe 711, Dar es Salaam.
Akizungumza leo Novemba 20, 2026 jijini Dar es Salaam wakati Waziri wa Ardhi Zanzibar, pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, Ardhi na TEHAMA ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar,
walpotembelea Ofisi za Makao Makuu ya NHC, Kambarage House, Dar es Salaam.
kwa ajili ya kujifunza masuala mbalimbali ya utendaji ikiwemo ujenzi miradi ya kimkakati inayotekelezwa na shirika hilo.
Waziri wa Ardhi Zanzibar, Rahma Kassim Ally, amesema ziara hiyo imekuwa fursa muhimu ya kujifunza namna NHC inavyotekeleza miradi ya makazi kwa kuzingatia ubora, ubunifu wa kisasa, miundombinu rafiki na mahitaji halisi ya wananchi.
Ameeleza kuwa kinachovutia katika miradi hiyo ni namna ilivyosanifiwa kuendana na mahitaji ya makazi, huku uwepo wake ukiwa na mchango mkubwa katika kubadilisha mandhari ya maeneo husika na kuyafanya kuwa ya kisasa.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC), Sultani Saidi Suleimani, amesema miradi waliyoitembelea imekuwa chachu ya maarifa kwao, akieleza namna NHC inavyopanga, kusanifu na kutekeleza miradi kuwa na mifano wanaoweza kuutumia katika kuboresha shughuli zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, amewashukuru viongozi na wajumbe wa ZHC kwa kutembelea miradi hiyo, akieleza kuwa shirika hilo litaendelea kuwa tayari kushirikiana na taasisi nyingine katika kubadilishana uzoefu na kuendeleza sekta ya nyumba nchini.
Aidha, ameahidi kutembelea Zanzibar kujionea shughuli zinazofanywa na ZHC, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano na kujifunza.
Ziara hiyo imelenga kuimarisha mahusiano ya kitaasisi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, kubadilishana uzoefu katika uendelezaji wa miradi ya nyumba, uwekezaji na mikakati ya kuongeza upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi
Katika mradi wa Golden Premier Residence (GPR), wajumbe walijionea maendeleo ya ujenzi pamoja na kupata maelezo ya kina kuhusu usanifu wa majengo, viwango vya ubora na matumizi ya teknolojia za kisasa zinazotumika katika ujenzi wa makazi.
Katika mradi wa Kawe 711 walipata fursa ya kutathmini hatua za utekelezaji, ubora wa ujenzi na namna mradi huo unavyolenga kuongeza upatikanaji wa makazi ya kisasa, salama na yenye mazingira rafiki kwa wananchi