Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesema Kanisa lina nafasi muhimu katika kuimarisha malezi na maadili ya jamii, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto ya mmomonyoko wa maadili.

Kapinga ametoa kauli hiyo Novemba 19, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Kichungaji cha Vijana cha Jimbo Katoliki la Mbinga, mkoani Ruvuma.

Katika harambee hiyo, Waziri Kapinga aliungana na baadhi ya viongozi, wadau wa Jimbo hilo na marafiki kuchangisha zaidi ya Sh milioni 124. Fedha hizo zikiunganishwa na michango ya waumini wa Kanisa, jumla ya fedha zilizopatikana zilifikia Sh milioni 440, kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa kituo hicho kinachokadiriwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni moja.

Amesema taasisi za dini, hususan Kanisa Katoliki, zina mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye maadili mema kupitia mafundisho, malezi na ushauri unaotolewa kwa waumini na vijana.

Amesisitiza kuwa waumini wa Kanisa Katoliki wana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika kulisaidia Kanisa kutekeleza majukumu yake, ikiwemo kuimarisha malezi ya vijana na kuwajenga katika misingi bora ya maisha.

Aidha, amesema ataendelea kuwa sehemu ya juhudi za kusaidia na kuunga mkono masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha huduma na shughuli za Kanisa, akieleza kuwa ushiriki huo ni muhimu katika kuchangia maendeleo ya jamii.